Sharti pekee la mwanafunzi kupata cheti cha kuhitimu elimu ya msingi
na sekondari nchini lilikuwa kuhudhuria shuleni, kufanya mitihani na
kufaulu, lakini sasa limeongezwa la kupanda miti ambalo halina uhusiano
na masomo darasani.
Kuanzia mwakani, moja ya masharti ya mwanafunzi kupewa cheti cha
kuhitimu elimu ni kuukabidhi uongozi wa shule mti alioupanda siku ya
kwanza alipoanza masomo na akautunza kipindi chote cha masomo.
Sharti hilo lilitangazwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba aliposhiriki mpango wa
upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo Kata
ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa akiongozana na viongozi wa mkoa.
Source: Mwananchi