Wadau wajadili upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Wadau wa mazingira wamekutana mjini Bagamoyo kujadili changamoto za upatikanaji wa fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianch... thumbnail 1 summary
Wadau wa mazingira wamekutana mjini Bagamoyo kujadili changamoto za upatikanaji wa fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo nchini. 

Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Forumcc, Oxfam, Care-Tanzania, ACSAA, FAO na IUCN ulilenga kuwajengea uwezo wadau hao namna ya kupata fedha kutoka katika Mfuko wa Fedha za Kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi (GCF).

Tanzania imeshapata kiasi cha dola za kimarekani 300,000 kutoka katika mfuko huo wa GCF kwaajili ya kujiandaa kupata fedha za kuhimili na kukabilana na mabadiliko ya tabianchi lakini changamoto kadhaa zinakwamisha upatikanaji wa fedha hizo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. 

Wadau waliainisha changamoto mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo katika kuandika miradi, uratibu wa pamoja na kukosekana na mfumo mzuri wa kupeana taarifa sahihi juu ya namna bora ya kuomba fedha kutoka katika mfuko huo.

Pamoja na sekta ya Kilimo kuchangia 25% ya pata la ndani la taifa na 24% ya pato la nchi la taifa ambapo zaidi ya 80% ya watanzania wanajihusisha na shughuli za kilimo bado sekta hii inakabiliwa na athari za mabadaliko ya tabianchi.

“Ili kupunguza athari hizo kunahitajika fedha za kukabiliana nazo, lakini upatikanaji wa fedha umekua ni changamoto kubwa. Utafiti wetu katika sekta ya Kilimo, mifugo na Uvuvi unaonyesha sekta hizi hupata fedha kidogo zinazopelekwa katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.” Anasema Mkurugenzi wa Forumcc, Rebecca Muna na kuongeza:

“Fedha kidogo zinapelekwa kwenye halmashuri na kushindwa kuleta mabadiliko chanya katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi” 

Katika mkutano huo Forumcc walishauri serikali kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo kwa kupeleka kiasi kikubwa kwenye miradi ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uelewa na kuingiza masuala hayo katika mipango na bajeti kwa ngazi zote.
Washiriki wa mkutano huo wakiendelea na majadiliano