UVUNAJI WA MITI MILIMA MATOGORO KUKAUSHA MTO RUVUMA, LUHIRA

Na Daniel Mbega, Songea MVUA zilikuwa zikimtendea haki Josephat Komba, mkulima katika kijiji cha Ndilima Litembo wilayani Songea, waka... thumbnail 1 summary
Na Daniel Mbega, Songea
MVUA zilikuwa zikimtendea haki Josephat Komba, mkulima katika kijiji cha Ndilima Litembo wilayani Songea, wakati pepo za kusi zilipovuma vyema na hivyo shamba lake la mpunga kupata maji ya kutosha yaliyompa mavuno mengi. Lakini hana uhakika kama atapata bahati kama hiyo msimu ujao.

"Zamani, hatukuwa na mashaka kuhusu hali ya hewa," anasema Komba, akiwa shambani kwake kilometa kadhaa kutoka Songea mjini. "Lakini hivi sasa, tatizo ni kubwa mno."
Komba anaitazama Milima Matogoro kwa masikitiko, na kujiuliza kama mabadiliko hayo ya hali ya hewa yameletwa na Mungu au wanadamu.
"Tumesikia mara kadhaa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, lakini nikwambie ukweli, miaka ya nyuma milima hii unayoiona hapa ndiyo ilikuwa mkombozi wetu. Tuliitegemea sana kwa ajili ya kuleta mvua, sasa hatujui kama ni laana ya Mungu au ni binadamu ndio tunaosababisha majanga haya," anasema.
Komba anasema, zamani walikuwa wakipanda kwa wakati na mvua zilinyesha katika kipindi kile kile. "Lakini tangu walipoanza kufyeka miti kwenye milima hii, kila kitu kimebadilika. Nadhani wameikasirisha miungu."
Misimu kadhaa iliyopita, mvua zikaanza kuadimika. Mara kadhaa mpunga wake ulikomaa bila unyevu; karibu theluthi ya mimea yake ilikauka kwa ukame na hata Mto Ruvuma ambao amekuwa akiutegemea umekuwa hauna maji ya kutosha hata nyakati za masika.
Mabadiliko hayo ya ajabu ya hali ya hewa ndiyo ambayo wanasayansi wa mazingira wanaamini kuwa ni madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa. Wakati mwingine kunaweza kuwa na ukame, lakini msimu mwingine mvua zinaweza kuwa nyingi kiasi cha kuleta mafuriko hivyo kushindwa kulima.
Komba analalamika kwamba, uchomaji wa moto kwenye msitu wa milima hiyo ni sababu nyingine inayoondoa hali ya asili ya milima hiyo ya Matogoro na hivyo kuleta wasiwasi mkubwa kwamba mito mikuu kama Ruvuma, Luhira na Luwegu itatoweka katika miaka michache ijayo.
Sehemu kubwa ya msitu wa Milima ya Matogoro imebakia vipara kutokana na uvunaji wa miti ya kigeni (exotic trees) kama Misindano (Pines) na Mikaratusi (Eucalyptus) ambayo wataalamu wa hifadhi ya vyanzo vya maji wanasema inayonya maji mengi.
Mhandisi Jaffari Yahaya wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Manispaa ya Songea (SOUWASA) anasema kwamba kuwepo kwa ukosefu wa maji wakati wa kiangazi katika Manispaa ya Songea kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya miti ambayo ipo katika misitu ya milima Matogoro ambayo hunyonya maji kwa kiwango kikubwa kwa kipindi cha mwaka.
“Miti hii inatakiwa ivunwe yote kama kweli tunataka vyanzo vya maji viendelee kudumu kwenye milima hii, vinginevyo kuna hatari ya maji kukauka na hivyo mito mikuu ukiwemo Ruvuma unaoanzia kwenye milima hii kutoweka,” anasema Eng. Jaffari.
Msitu wa Milima ya Matogoro wenye ukubwa wa kilometa za mraba 48 ulipitishwa na Serikali ya Tanganyika mwaka 1951 chini ya Notisi ya Serikali Na. 260 kuwa kama shamba la mbao na kati ya mwaka 1967 – 1979 serikali ikapanda miti ya kigeni katika eneo la hekta 867 ambazo awali zilikuwa zikikaliwa na wananchi kabla ya kuhamishwa.
Lakini mwaka 2000 Serikali ikautangaza msitu huo kama wa Hifadhi ya Vyanzo vya Maji, ambapo SOUWASA ina jumla ya vyanzo tisa vinavyotumika kukusanya maji yanayotumiwa na Manispaa ya Songea huku pia ukiwa vyanzo vya mito mitatu.
Mito hiyo muhimu ni Ruvuma wenyewe, Mto Luhira ambao unamwaga maji yake kwenye Mto Ruhuhu (mto mkuu unaomwaga maji Ziwa Nyasa), na Mto Luwegu ambao unamwaga maji yake kwenye Mto Rufiji katika makutano yake mkoani Morogoro.
“Tuliamriwa kuvuna haraka miti yote ya kigeni inayoonekana kunyonya maji na kupanda miti ya asili, lakini zoezi hili linaonekana kuwa gumu kwa sababu linahitaji bajeti kubwa,” anasema Abednego Sakafu, Meneja wa Shamba la Miti Matogoro.
Bila kueleza ni gharama kiasi gani zinazohitajika, Sakafu anasema kuna changamoto nyingi zinazowakabili kiasi kwamba wameshindwa kufikia malengo ya kuvuna miti yote kama walivyokuwa wameagizwa.
“Tulitakiwa tuwe tumevuna miti yote kufikia mwaka 2006, lakini bado zoezi ni gumu,” anasema na kuongeza kwamba, pamoja na kasi ya uvunaji miti hiyo kuwa kubwa kwa kuvuna hekta 827 mpaka sasa kati ya 867, upandaji wa miti rafiki ambayo ni ya asili kama miombo, migwina, minyenda na mikusu unasuasua kutokana na sababu mbalimbali.
Mojawapo ya sababu zinazotajwa ni kuchipua kwa haraka kwa miti ya kigeni inayovunwa pamoja na miti mingine kuota kutokana na kupukutiza mbegu, lakini pia miti ya asili imekuwa ikichelewa kukua tofauti na ile ya kigeni.
“Miti ya kigeni haikui haraka kama ya kigeni na kila mwaka watu wanapochoma msitu wa milima hiyo miti hii michanga huteketea na kulifanya zoezi kuwa gumu. Kung’oa visiki vya miti ya kigeni ni zoezi jingine ambalo serikali inapaswa kuliangalia kwa makini na kutenga fungu la kutosha kama kweli inataka miti hii iondoke,” anaongeza Sakafu.
Kutokana na uvunaji huo wa miti pamoja na uchomaji moto, eneo kubwa la milima ya Matogoro limeathiriwa na mmomonyoko wa udongo hali inayoleta ugumu pia wa upandaji wa miti hiyo ya asili kwani haiwezi kukua kwa kukosa rutuba.
Ofisa Maliasili wa Mkoa Ruvuma Enock Buja anasema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini (TAFORI), imebaini kuwepo kwa aina kadhaa ya miti ambayo kwa kiwango kikubwa inanyonya maji mengi.
Anaitaja miti hiyo kuwa ni Mikaratusi ya jamii ya Camaldulensis ambayo hunyonya maji kiasi cha milimita 1,240 kwa mwaka na Mikaratusi aina ya Microrhea inayonyonya maji milimita 1,050 kwa mwaka.
“Mikaratusi ya aina ya Patula nayo hunyonya maji kiasi cha milimita 665 kwa mwaka. Mingi imekwishaondolewa isipokuwa tatizo la kujiotea kila inapovunwa ndilo linalosumbua,” anaongeza Buja.
Katika utafiti huo imeelezwa kuwa ipo miti mingine kama Mgunga na Mvile inayoelekea kutumia maji mengi kuliko Mikaratusi.
 
Mgongano wa Sera
Lakini wakati Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kuuacha Msitu wa Matogoro na kuanzisha shamba jingine la Miti katika kijiji cha Wino ili kupisha uvunaji wa miti hiyo kutunza vyanzo vya maji, mnamo Machi 2011 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa Luoga, alipiga marufuku ukataji miti kwenye milima hiyo.
Dk. Luoga alisema kwamba, ukataji huo wa miti unaharibu mazingira pamoja na vyanzo vya maji, hivyo kuwa tishio la kukauka kwa chanzo kikuu cha Mto Ruvuma, Luhira na Luwegu pamoja na mito mingine midogo kama Lipasi, Liwoyowoyo na Mkurumusi.
“Hii nayo ni changamoto kubwa katika uhifadhi wa maji, maana kila wizara inakuja na sera zake japokuwa serikali ni hiyo hiyo moja. Tunahitaji kuvihifadhi vyanzo hivi na uvunaji wa miti, ambayo mbali ya kunyonya maji pia inasababisha maji kuwa na tindikali, ulikuwa unalenga kuhifadhi hayo hayo mazingira,” anasema Reginald Mapunda, Ofisa wa Bonde la Ruvuma.
Mapunda anakiri kwamba uvunaji huo wa miti bila mkakati madhubuti wa kupanda mingine unahatarisha uhai wa Bonde la Ruvuma, lakini pia ubora wa maji ni jambo jingine ambalo serikali inafanya jitihada kulitekeleza.
Hofu yake nyingine ni wananchi wanaolima karibu ama kando kando ya vyanzo vya maji, ambao anasema, wanachochewa na wanasiasa na watunga sera licha ya wanasiasa hao kutambua sheria zilizopo kuwa zinakataza watu kufanya shughuli jirani na vyanzo vya maji.
“Sheria ya Maji inasema hairuhusiwi kufanya shughuli zozote ndani ya meta 200 kutoka kilipo chanzo cha maji na Sheria ya Mazingira inasema shughuli zozote zisifanyike ndani ya meta 60 kila upande. Yote haya yana manufaa, lakini bado wanasiasa wanawahimiza wananchi kulima mabondeni kando ya mito bila kujali sheria zilizopo,” anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, anakiri kwamba kuna changamoto kubwa katika kutunza vyanzo vya maji, hasa katika Milima ya Matogoro, kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kando ya milima hiyo.
Anasema hali ya uchomaji moto misitu ya milima hiyo inatishia vyanzo vya maji na kwamba serikali yake inafanya  juhudi kupambana na uharibifu huo pamoja na jitihada za kuhamasisha upandaji miti.
“Suala si kupanda miti Matogoro pekee, bali katika maeneo yote na ilikwishakubaliwa kuwa kila wilaya ipande miti 1,500 walau kila mwaka. Hii itasaidia kuboresha mazingira pamoja na kupambana na joto na hewa ya ukaa hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema.