Asalimisha zana za ushirikina kanisani

Na Berensi Alikadi, Bunda MAMIA ya wananchi wa mji wa Bunda mkoani Mara jana walimiminika katika Kanisa la EAGT lililoloko Mtaa wa ... thumbnail 1 summary

Na Berensi Alikadi, Bunda

MAMIA ya wananchi wa mji wa Bunda mkoani Mara jana walimiminika katika Kanisa la EAGT lililoloko Mtaa wa Chiringe, kumshuhudia kijana mmoja, Musa Joseph (18), akisalimisha zana zake alizokuwa akifanyia uchawi.

Ilikuwa majira ya saa nane mchana kanisani hapo, ambapo wananchi kutoka maeneo mbalimbali walimiminika baada ya taarifa kuenea kuwa kijana huyo aliahidi kusalimisha vitu mbalimbali zikiwamo tunguli pamoja na mbwa ambaye alikuwa akimtumia kusafiria.

Mchungaji wa kanisa hilo, Deoras Elia, alisema kuwa kijana huyo awali alikuwa akisali katika kanisa hilo lakini  baadaye aliacha na kwamba wiki mbili zilizopita aliwafuata baadhi ya viongozi wa kanisa hilo na kuwaambia kuwa  alikuwa na mpango wa kuachana na kazi hiyo akitaka kuokoka.

Mchungaji huyo alieleza kuwa baada ya viongozi wa kanisa kupata taarifa hizo waliamua kumfuatilia kijana huyo na kuzidi kumuombea ambapo aliahidi kupeleka vifaa vyake hivyo kanisani hapo.

Akizungumza na Tanzania Daima nje ya kanisa kabla ya kusalimisha zana zake hizo, kijana huyo alisema kuwa kwa hivi sasa anaishi na bibi yake aitwaye Tabu Mangedele katika Mtaa wa Nyasura  na kwamba alianza kazi hiyo ya uchawi mwaka 2005.

“Nilipata utaalamu wa uchawi huo kutoka kwa bibi yangu aitwaye Rebeka Magendele aishiye Nyakato jijini Mwanza, Bibi alinipa vifaa vya kufanyia kazi kama fisi watano wote wa kike, kibuyu na ungo, ambavyo nilikuwa navitumia kuruka kwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya shughuli za uchawi,” alisema.

Baada ya mahojiano hayo aliingia kanisani na alipopewa nafasi ya kutoa ushuhuda alisema kuwa alikuwa mkurugenzi msaidizi wa wachawi ambapo mkurugenzi mkuu kwa upande wa Tanzania yuko wilayani Ukerewe akiishi katikati ya kisiwa na kwa upande wa Afrika mkuu wa wachawi anaishi nchini Nigeria.

Kuhusu maeneo waliyokuwa wanakwenda kufanya vitendo vya kichawi, kijana huyo aliyataja kuwa ni Mbezi Mwisho, Kawe, Mwenge jijini Dra es Salaam, Zanzibar na Mtwara.

Mara baada ya kutoa maelezo hayo, alitoa vifaa vyake na kuvikabidhi kwa mchungaji wa kanisa hilo na kisha vikachomwa moto huku  mbwa wake akiondoka na kuelekea kusikojulikana baada ya mchungaji huyo kudai kuwa huyo sasa ni mbwa wa kawaida na wala si mbwa wa kichawi tena.

Chanzo: Tanzania Daima