Mussa Mwangoka, Sumbawanga.
JESHI la polisi mkoani Rukwa
linashikilia watu wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi kwa tuhuma za
kuhusika katika tukio la mauaji ya wafanyabiashara wawili na kupora
mamilioni katika kijiji cha Kaengesa wilayani Sumbawanga.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa Jacob Mwaruanda alisema jana ya simu
kuwa tukio hilo lilitokea alfariji kuamika jana ambapo kundi la watu
hao hao walifanya mauaji kwa nyakati tofauti katika eneo la Kaengesa na
kijiji cha Lula.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinadai kuwa kati ya watu
wawili waliokufa mmoja ndiye alitambuliwa kuwa ni Abineli Kasonje mkazi
wa Lula ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na kumjeruhi mke wake kwa
panga wakati mabishano ya kulazimishwa awape pikipiki yake ili watoroke
nayo.
Mwaruanda alisema kuwa kabla ya kuvamia nyumba ya Kasonje na
kumuua, awali waliiteka kwa muda mfupi nyumba moja ya kulala wageni
iliyopo eneo la Kaengesa ambapo waliingia chumba kimoja hadi kingine
ambako waliwalazimisha wageni waliokuwa wamelala katika vyumba hivyo
kutoa fedha, simu na vingine vya thamani sambamba na kuwachapa na
viboko.
Kamanda Mwaruanda alisema kuwa wakati wakiendesha operesheni hiyo
watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walimpiga risasi na kumuua
mfanyabiasha mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye
inaelezwa alifika kijijini hapo kwaajili ya kununua mazao ya mahindi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mfanyabiashara huyo anadaiwa kutoka mji
mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambaye aliiuawa kwa kupigwa
risasi iliyopata kifuani na kufariki dunia akiwa chumbani baada ya
kukosa msaada wa aina yoyote.
Hata hivyo kufuatia kusikika kwa milio ya risasi na kelele za watu
walijitokeza wasamaria wema ambapo iliwabidi majambazi hao kukimbia na
kuelekea kitongoji cha jirani cha Lula na kuvamia nyumba ya Kasonje
ambako walimuua mtu huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya polisi kupata taarifa hiyo
walifanya msako ambapo walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa wawili ambao
majina yao yanahifadhiwa walionanaswa katika kijiji cha Msanzi umbali
wa zaidi ya kilometa 20 kutoka eneo la tukio.
Mwisho.