na Danson Kaijage, Mpwapwa
WANAWAKE wa
Kijiji cha Iyoma, wilayani Mpwapwa wanalazimika kutembea saa mbili hadi tatu
kwa ajili ya kutafuta maji kwa matumizi ya kawaida.
Hayo yalielezwa
na wanakijiji wa kijiji hicho kwenye mkutano wa hadhara na Mkuu wa Wilaya ya
Mpwapwa, Christopher Kangoye.
Mkuu huyo
alilazimika kukutana na wananchi kwa lengo la kutoa elimu, juu ya uzalishaji wa
kipato na utunzaji wa mazingira wilayani hapo.
Wanakijiji hao
walisema pamoja na serikali kuwahimiza kuwa na maendeleo, lakini wanasahau kuwa
bado wanakosa maji ya uhakika ambayo ni huduma muhimu katika maisha ya kiumbe
hai.
Mmoja wa
wananchi ambaye alijitambulisha kwa jina la Jackson Noah, alisema kuwa kitendo
cha kukosa maji katika maeneo yao, kinasababisha wake zao kuyafuata umbali
mrefu.
Noah alisema
kitendo cha kinamama kuamka saa kumi alfajiri kufuata maji kwa umbali mrefu, ni
sababu kubwa ya kukosekana kwa maendeleo kwani nguvu kazi inapotelea katika
kufuata maji.
Naye Zaina
Bakari alisema kijiji hicho kwa miaka kumi sasa wananchi wanatumia maji ya
kwenye madimbwi wanayogombania kati yao na wanyama.
Zaina alisema
kutokana na tatizo hilo, uzalishaji umepungua kijijini hapo kutokana na
akinamama wengi kujikita kwenye utafutaji maji badala ya kwenda kwenye shughuli
za uzalishaji.
Chanzo: Tanzania Daima