MAPIGANO YA WAMASAI, WASONJO YAJERUHI 7

Mussa Juma, Arusha WATU saba wamejeruhiwa kwa risasi, huku mbuzi na ng’ombe zaidi ya 300 kuporwa na nyumba 11 kuteketezwa kwa mot... thumbnail 1 summary
Mussa Juma, Arusha

WATU saba wamejeruhiwa kwa risasi, huku mbuzi na ng’ombe zaidi ya 300 kuporwa na nyumba 11 kuteketezwa kwa moto katika mapigano ya kikabila ya kugombea ardhi baina ya Wasonjo na Wamasai wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Mapigano hayo, yalilipuka tena jana alfajiri takriban miezi sita baada ya yale ya awali yaliyosababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa Februari mwaka huu.

Mapigano ya sasa yametokea katika kitongoji cha Naam, Kata ya Enguserosambu, Tarafa la Loliondo, wilayani Ngorongoro, baada ya baadhi ya watu wanaodaiwa ni wa jamii ya Kisonjo kuvamia kitongoji hicho kwa madai kuwa eneo hilo ni la kwao na hawataki Wamasai kuandikishwa katika Sensa wakiwa katika eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Zuberi Mwombeji walithibitisha kupata taarifa za mapigano hayo, lakini wote walieleza kutokuwa na taarifa kamili za mapigano hayo kwani katika eneo la mapigano hakuna mtandao wa simu.

Mkuu wa wilaya, ambaye yupo mjini Arusha kikazi, alisema tayari ujumbe wa Serikali umetumwa katika kitongoji hicho kupata taarifa na kujionea uharibifu ambao umetokea.
Naye Kaimu Kamanda, Mwombeji alisema pia jana asubuhi, kikosi cha polisi kilikuwa kimetumwa katika eneo la mapigano.

“Ni kweli kuna vurugu huko, tumewatuma polisi wamekwenda ila tatizo hakuna mawasiliano,” alisema Mwombeji.

Hata hivyo, wakizungumza kutoka Loliondo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema watu saba walikuwa wamejeruhiwa kwa risasi, wanne wakiwa ni wa familia moja.

Mratibu wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilaya ya Ngorongoro (NGONET), Samweli Nang’irya alisema taarifa za awali walizozipata ni kuwa boma lililovamiwa ni la Ole Masangori ambapo yeye na vijana wake, watatu wamejeruhiwa.

“Mzee mwenyewe tumeelezwa kachomwa singe ya bunduki wakati vijana wake, wamejeruhiwa kwa risasi sambamba na vijana wengine watatu ambao ni wakulima wa jamii ya Kiiraq,” alisema Nang’irya.
Alisema taarifa za awali ambazo walipata jana ni kuwa ng’ombe zaidi ya 200 na mbuzi 160 wameporwa, pia kuna watu ambao hawajulikani walipo.

“Muda huu gari la wagonjwa kutoka Hospitali ya Wasso, Loliondo limeenda kuwachukuwa majeruhi na kujua athari za tukio hilo,” alisema Nang’irwa.

Makamu Mwenyekiti wa jukwaa la wanataaluma Wilaya ya Ngorongoro, Onesmo Ole Ngulumwa alisema matatizo ya ardhi Ngorongoro ni ya muda mrefu lakini Serikali imeshindwa kuyapatia ufumbuzi.
Alisema Serikali pia ilipaswa kutoa elimu ya Sensa mapema kabla ya zoezi kuanza kwani mgogoro wa sasa unachangiwa pia na uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na Sensa.

Migogoro ya ardhi imekuwa ikitokea mara kwa mara baina ya jamii ya Wasonjo na Wamasai Ngorongoro, na tangu mwaka 1974 vikao mbalimbali vya usuluhishi vimefanywa na viongozi wa juu wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali bila ya mafanikio.

Mwafaka ambao ulidhaniwa ungetoa suluhisho uliendeshwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Marehemu Edward Sokoine aliyewasuluhisha kimila kwa mtoto wa Kimasai na Kisonjo kunyonya kwa wanawake wa makabila hasimu ili kujenga uhusiano, lakini hata hivyo ilishindikana kupatatikana mwafaka.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikiahidi kutatua mgogoro huo, kwa kupima ardhi ya Ngorongoro na kutenga maeneo ya kilimo na mifugo hatua ambayo hadi sasa bado haijafanyika licha ya kuahidiwa mara kadhaa.
Chanzo: Mwananchi