NJAA YANYEMELEA KIJIJINI KWA JK

na Julieth Mkireri, Bagamoyo NJAA kali inaweza kuwakumba wakazi wa kata ya Msoga, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, ndani ya miezi mitat... thumbnail 1 summary

na Julieth Mkireri, Bagamoyo
NJAA kali inaweza kuwakumba wakazi wa kata ya Msoga, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, ndani ya miezi mitatu ijayo kutokana na kupata mavuno kidogo kwa mwaka huu.
Hayo yalibainishwa na Ofisa Kilimo na Mifugo wa Kata hiyo, Donald Kiende, katika kijiji cha Msoga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya chakula katika kata hiyo.
Kiende alisema kuwa malengo ya kilimo cha mahindi katika kata hiyo ilikuwa ni kulima ekari 5,250 kwa mwaka huu lakini zimelimwa 3,509.
Alisema kuwa iwapo wakazi hao wangelima kwa wingi, wangefanikiwa kuvuna tani 19,200 ambazo zingetosheleza kwa chakula cha mwaka mzima.
Kwa mujibu wa ofisa kilimo huyo, alisema kuwa utafiti unaonyesha kuwa mtu mmoja ana uwezo wa kula gunia tatu kwa mwaka, jambo ambalo lilitakiwa kuvunwa gunia 31,100 kulingana na idadi ya wakazi 10,500 wa kata hiyo.
Aliwaasa wakazi wa kata hiyo kuacha tabia ya kuuza mazao kwa walanguzi kwani kufanya hivyo wanaweza kupunguza hata kiasi cha chakula kilichopo na hivyo kukumbana na njaa mapema.
Chanzo: Tanzania Daima