WALIOVAMIA TENGEFU KILOMBERO WATAKIWA KUONDOKA

na Asha Bani WATU waliovamia na kuishi katika pori Tengefu la Kilombero wametakiwa kuondoka kwenye eneo hilo kwa hiari yao kabla ya kufika... thumbnail 1 summary
na Asha Bani
WATU waliovamia na kuishi katika pori Tengefu la Kilombero wametakiwa kuondoka kwenye eneo hilo kwa hiari yao kabla ya kufika Agosti 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, George Matiko, azimio hilo lilifikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika Agosti 14, mwaka huu kati ya uongozi wa wilaya za Kilombero na Ulanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi.
“Nia ya kikao hicho ilikuwa ni kuweka mikakati ya kutekeleza azma ya serikali ya kuwataka wavamizi katika pori hilo kuondoka,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema kuwa kikao hicho kilikubaliana kuwa ifikapo Septemba 8, mwaka huu kazi ya kuwatoa wavamizi hao ambao bado watakuwepo katika pori hilo itaanza mara moja.
Kwamba kazi hiyo ya kuwaondoa itatekelezwa kwa pamoja na kamati za usalama ngazi ya mkoa na wilaya za Ulanga na Kilombero, kikosi dhidi ya ujangili, askari polisi na askari kutoka pori la akiba la Selous.
“Hadi sasa wananchi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa pori hilo na manufaa yatakayopatikana kama litaachwa wazi. Wanavijiji wanaopakana na pori hilo wameonyeshwa mipaka baina ya vijiji vyao na pori,” ilifafanua taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, mipango imekamilika ya kuiwekea mifugo alama (brands) kwa lengo la kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyoko katika Bonde la Kilombero, kazi inayoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Ilisema kuwa kazi ya kutambua mipaka, kufyeka na kuweka alama (beacons) zinaendelea kwa pamoja katika vijiji 105 vya wilaya za Ulanga na Kilombero na zinategemewa kukamilika Agosti 27, mwaka huu.
Iliongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii iliahidi kuchangia kiasi cha sh 106,500,000 ili kuharakisha utekelezaji wa kuimarisha mipaka.
Chanzo: Tanzania Daima