MBWA MWITU 40 WAUAWA KWA MOTO HIFADHI YA SERENGETI

Na Charles Ngereza Zaidi ya mbwa mwitu 40 wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya mapango katika vijiji vya Kertalo na Orkiu mpakani mwa Hifa... thumbnail 1 summary
Na Charles Ngereza
Zaidi ya mbwa mwitu 40 wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya mapango katika vijiji vya Kertalo na Orkiu mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Habari kutoka Loliondo zinaeleza kuwa mbwa mwitu hao waliuawa na watu wasiojulikana ambao wanadaiwa kujaza kuni ndani ya mapango wanayoishi wanyama hao na kuwasha moto.

Imeelezwa kuwa baada ya kuwasha moto, wauaji waliyafunika mapango hayo  kwa mawe na kuwateketeza wanyama hao wanaotajwa kuwa katika hatari ya kutoweka duniani.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elius Wawa Lali, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza uchunguzi wa kubaini wahusika unaendelea.

“Ni kweli tukio hilo limetokea na  kwa sasa vyombo vya  ulinzi na usalama vinalifanyia uchunguzi na ukikamilika tutawapa taarifa kamili," alisema.

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo walisema siku chache kabla ya mbwa mwitu hao kuuawa, watu hao waliua ndama wanne na mbuzi 157 mali ya wanakijiji.

Mbaaryo Papalai alisema kuwa mbwa mwitu hao  wamekuwa wakitishia usalama wa mifugo yao na kila walipoua mbuzi hakuna fidia yeyote au kifuta machozi wanachopata kutoka serikalini.

“Mimi sijui ni nani kawaua lakini ametusaidia kwani hao mbwa ni hatari wamekula mbuzi wangu kumi na sita mwezi wa tisa mwaka huu na hakuna chochote tunachopewa kama kifuta jasho,” alisema Papalai.

Chanzo: Nipashe