na Bertha
Mwambela, Tanga
WAZIRI wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepiga marufuku wafanyakazi wa wizara yake
kusafiri kwa ndege katika daraja la kwanza wanapokwenda nje ya nchi, akidai huo
ni uharibifu wa fedha za umma.
Akizungumza na
waandishi wa habari mkoani hapa jana, Dk. Mwakyembe alisema kuanzia sasa
wafanyakazi wote wa serikali walioko chini ya wizara yake ni marufuku kusafiri
kwa ndege wakitumia daraja la kwanza na kuonya kuwa atakayebainika fedha yake
itakatwa kwenye malipo yake.
Alisema
anayetakiwa kusafiri na ndege daraja la kwanza ni rais pekee na si watendaji
wengine, jambo alilodai kuwa hata kwenye nchi nyingine wanawashangaa kwa
utaratibu wanaoutumia wa kuharibu fedha zinatokana na kodi za wananchi.
“Inanishangaza
sana kuona baadhi ya watendaji hawana uchungu na fedha za Watanzania, sasa
nasema marufuku kuanzia leo kwa wafanyakazi wote walioko chini ya Wizara ya
Uchukuzi, kusafiri kwa ndege daraja la kwanza, naomba wote tutumie daraja la
pili,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema kuwa
lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanajipanga ili kukabiliana na changamoto
mbalimbali ambazo zimepangwa kuboreshwa na kila mtu kuwajibika katika nafasi
yake ili kuweza kufikia malengo ya kuboresha sekta hiyo.
Waziri
Mwakyembe aliongeza kuwa, hatakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote ambae hataweza
kufikia malengo ya utendaji kazi waliojipangia kama wizara, ili kukabiliana na
ushindani wa nchi jirani za Afrika Mashariki.
Katika hatua
nyingine, waziri huyo alisema anao uhakika wa kusonga mbele kwa bandari ya
Tanzania kwani bodi ya wakurugenzi aliyoiteua hivi karibuni ana imani nayo.
Chanzo: Tanzania Daima