Mzungu atoa ushuhuda mitutu ya bunduki ilivyoua tembo 10

Dotto Kahindi Vitendo vya ujangili nchini Tanzania vimezidi kuongezeka siku hadi siku na kutoa picha mbaya kwa mataifa mengine ndani na nj... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi
Vitendo vya ujangili nchini Tanzania vimezidi kuongezeka siku hadi siku na kutoa picha mbaya kwa mataifa mengine ndani na nje ya bara la Africa huku hali hiyo ikionekana kuwa mfupa mgumu uliozishinda mamlaka mbalimbali hapa nchini.
Kwa kipindi kirefu Tanzania imekuwa ikijaribu kuficha hali halisi ya ujangili katika hifadhi zake lakini Mtalii wa uwindaji ambaye alitembelea nchini mwezi Agosti mwaka huu ameiumbua Tanzania kwa kutoa ushuhuda wa namna uwindaji unavyofanyika na mamlaka zikichekea hali hiyo.
Mtalii huyo wa uwindaji Paul Lavender katika barua yake aliiyoituma kwenye mtandao wa Bryan Christy, (mwandishi wa ripoti ya uchunguzi aliyoita ‘Blood Ivory’) anasema akiwa katika ziara yake nchini Tanzania katika hifadhi ya taifa ya Rungwa alishuhudia mauaji ya tembo yaliyofanyika bila huruma.
Anasema akiwa kwenye ziara hiyo chini ya waongozaji wa watalii wa uwindaji yeye pamoja na mke wake walishuhudia mauaji ya tembo yakiyofanyika waziwazi bila kificho na mamlaka husika kushindwa kuchukua hatua.
Katika siku yao ya kwanza hifadhini hali ilionekana kuwa shwari na kuiona sehemu ile kama mahala salama kwa wanyama jambo ambalo lilikuwa tofauti kabisa katika siku ya pili ambapo walisikia milio ya bunduki mfululizo umbali wa kilomita moja kutoka katika kambi yao mchana kweupe.
“Tulisikia milio ya silaha nzito za moto kwa zaidi ya mara 100 tena mchana kweupe, hali ambayo ilitupa wasiwasi na kushindwa kuamini kama mambo hayo yanaweza kufanyika katika nchi kama Tanzania” anasema Levender

Anasema kuwa muongozaji wao hata yeye pia alionekana kuteteleka na kukerwa na hali ile lakini hakuwa na namna ya kufanya na kuendelea kuwasihi wawe wavumilivu na watulivu kwa kuwa milio hiyo ya risasi ilikuwa ni kutokana na majangili ambao kawaida yao huja kuua wanyama na kuwaaacha watu salama, na kwamba hawatakuwa na madhara kwo.
Milio hiyo ilitulia kwa kipindi Fulani hawakuwa na budi kukubalina na ushauri wa mwongozaji wao lakini iliwashangaza sana kuona vitendo hivyo vikifanyika na kujikuta wakiishiwa nguvu baada ya kuambiwa kuwa muongozaji wa watalii wa uwindaji aliuawa na majangili mwaka jana katika eneo hilo hilo.
Anasema kuwa usiku ule ulikuwa wa mateso kwani milio ya bunduki iliendelea tena na mara hii hawakuwa na uvumilivu tena wakaamua kukimbilia kwenye gari ili waondoke maeneo yale kwa usalama wa maisha yao.
“Muongozaji wetu alipiga simu kwa mkuu wa hifadhi hiyo lakini hata hivyo hakuweza kufanya chochote kile kwa kuwa alikuwa ni mgeni (mpya) na kwamba hakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya eneo hilo” anasema Levender kwenye barua yake hiyo.
Hali hiyo iliwalazimu kupiga simu katika makao makuu ya kampuni ya Safaris ambapo baadae kundi la askari wanyama pori walikwenda wakiwa kwenye gari jipya la land cruiser katika kambi ya watalii hao ikiwa ni majira ya jioni na kuahidi kwenda kuchunguza kilichotokea kwenye milio ya bunduki asubuhi ya kesho yake.
“Haikuwa wazi na haikuingia akilini kwanini walikuja kwenye kambi yetu badala ya kwenda kupambana na majangili moja kwa moja waliokuwa wakifurumusha risasi na kuua wanyama tena jirani kabisa na tulipokuwa, badala yake wanasubiri kwenda kesho yake” alihoji Levender

Anasema asubuhi kulipokucha walikwenda na muongozaji wao hadi katika eneo la tukio ambako waliwakuta tembo 11 wakiwa chini wamekufa na kunyofolewa pembe zao mbaya zaidi wengine walikuwa ni watoto ambao waliuawa na kuachwa kwa kuwa hawakuwa na meno tayari.

“Tulihuzunishwa sana na hali tuliyoikuta baada ya kuwakuta tembo 11 wakiwa wamekufa, tembo wakubwa, watoto tena bila huruma, kwa sababu wanyama wadogo hata hawakuwa na pembe hizo lakini nao waliuawa, nilichukua picha nyingi tu za unyama huu” anasema Levender
Levender anasema kuwa askari waliofika eneo hilo walizunguka na kufanya uchunguzi wa awali na kubaini kuwa kulikuwa na majangili wapatao wanane au 10 ambao waliufanya usiku ule kama uwanja wa mapambano ya kivita.
Lakini mbaya zaidi ni kwamba watu hao walikuwa na baskeli walizotumia kama usafiri wao na hata alama za matairi ya baskeli zilikoelekea yalionekana.
Anaendelea kudai kuwa eneo ambalo mauaji hayo yalifanyika lilikuwa karibu sana takribani kilomita 800 kutoka katika kambi waliyokuwa wamefikia lakini cha kushangaza hakukuwa na jitihada zozote zile za kuwakamata waliofanya vitendo hivyo.
Anasema kuwa mbali na kuwa karibu na kambi yao pia mauaji hayo hayakufanyika mbali sana na kijiji ambako ndio majangili hao walionekana kuelekea, umbali wa maili 30 na kwamba kwa mazingira hayo isingekuwa rahisi kwa majangili hao kutoroka lakini bado walitoroka na mamlaka ukionyesha kutoshtushwa na hali hiyo.
“Tuliendelea kuzunguka kwa siku tatu zaidi ambapo tulikuta mizoga ya tembo wengine watatu ambao wameuawa hivi karibuni, muangozaji wetu amabye amekuwa katika hifadhi hiyo kwa muda mrefu alisema kuwa idadi ya tembo wanaouawa inazidi kuongezeka kila siku na kuna hatarai ya kuangamiza kabisa wanyama hao Tanzania” anasema Levender na kuongeza:
“Siku iliyofuata tuliambiwa kuwa askari wanyama pori wameweka mtego na kuvamia klabu cha pombe katika kijiji cha jirani ambako ilisadikiwa kuwa majangili walikuwepo wakinywa pombe lakini hata hivyo mtego huo haukufanikiwa”
Anasema kuwa ni jambo la ajabu kugundua kuwa majangili wanapata muda wa kujipongeza kwa kunywa pombe baada ya kazi nzito ya kuua tembo huku mamlaka ziking’aza macho jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa mtu yeyote mwenye akili timamu.
0655361266, kingkahindi@gmail.com