Changamoto
za uhaba wa wakufunzi wa masuala ya nyuklia sambamba na vifaa kwa ajili ya
mafunzo hayo barani Afrika vinatajwa kuwa kikwazo katika kuwaandaa wataalamu wa
sayansi ya nyuklia hali inayochangia ukosefu mkubwa wa wataalamu hao.
Njia
ya elimu kwa mtandao yaan E-learning inatajwa kama moja ya njia zitakazosaidia
uboreshwaji wa utoaji wa mafunzo hayo katika vyuo vikuu barani Afrika, lakini
changamoto kubwa iliyopo ni uhaba wa wakufunzi wa sayansi ya nyuklia na vifaa
vinavyohitajika katika mafunzo.
Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa ambaye licha ya
kusisitiza umuhimu wa njia hiyo pia anasema serikali ya Tanzania inafanya
jitihada kubwa za kuhakikisha inatengeneza mazingira yatakayorahisisha njia za
mafunzo, akitolea mfano wa ujenzi wa mkongo wa taifa ambao umerahisha kwa kiasi
kikubwa huduma za mawasaliano hivyo kuwezesha mafunzo kwa njia ya mtandao
kufanyika nchini.
Mkurugenzi
wa tume ya mionzi Tanzania Profesa Juma Mkilaha amesema mkutano huu una lengo
kuu la kujadili mkakati maalumu utakaoelekeza namna vyuo vitakavyoshirikiana
katika kutoa mafunzo ya sayansi ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kubadilishana
wakufunzi.
Nae
Mwenyekiti wa AFRA-NEST Profesa Shaukat Abdulrazak amesisitiza kuwa ili nchi za
afrika ziweze kupiga hatua katika sekta ya Nyuklia hazina budi kutia
mkazo katika masomo ya sayansi sambamba na kuboresha miundombinu.
Mkutano
huo wenye lengo la kujadili namna ya kuboresha utoaji wa elimu ya sayansi ya
Nyuklia katika vyuo vinavyotoa mafunzo hayo ili kukabiliana na changamoto ya
uhaba wa wataalamu wa nyuklia katika nchi za Afrika, unawakautanisha wataalamu
mbalimbali kutoka katika sekta za nyuklia na vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo ya
sayansi ya nyuklia kutoka katika nchi zipatazo 31 ambazo ni wanachama wa
umoja huo.