Mwindaji pori la Sikonge afanya unyanyasaji mkubwa kwa wananchi

BARAZA la Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limemkataa mwekezaji anayejishughulisha na uwindaji katika pori la... thumbnail 1 summary
BARAZA la Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limemkataa mwekezaji anayejishughulisha na uwindaji katika pori la misitu ya hifadhi iliyoko wilayani humo kwa vitendo vya unyanyasaji wananchi, kuuza wanyama na vitalu vya uwindaji  kiholela.

Akitoa taarifa ya uamuzi huo kwa niaba yaMadiwani, watendaji wa halmashauri na wananchi wote wa wilaya hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Robert Kamoga amesema wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji, ubabe, dhuruma, wizi na uonevu unaofanywa na wawindaji walioko katika mapori ya hifadhi wilayani humo.

Amesema wawekezaji hao wanajifanya miungu watu na hawajui kama mapori hayo  ni mali ya Serikali na msimamizi wake mkuu ni Serikali ya wilaya kupitia Baraza la madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo, kibaya zaidi hawatambui kuwa wako chini ya mamlaka ya serikali.

Mwekezaji huyo anayejulikana kwa jina la SHEN kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa kero kwa wananchi wanaoishi karibu na misitu hiyo ya hifadhi na anadaiwa kujimilikisha kwa nguvu hifadhi za misitu na  Koga.

Aidha mwekezaji huyo anadaiwa kuuza raslimali zilizoko katika hifadhi hizo huku akidai kuwa ana Ramani toka wizarani inayomruhusu kumiliki eneo lote la tarafa ya Kiwere na kufanya chochote anachotaka ndio maana anatoa vitisho vya kuwahamisha kwa nguvu wananchi wote wanaoishi karibu na misitu hiyo wilayani humo.


Mwenyekiti wa CCM wilayani Sikonge ,Bw.Abisai Mbogo amepongeza uamuzi huo wa Madiwani na kuongeza kuwa hakuna Serikali inayoweza kuruhusu mikataba ya namna hiyo ya kumiliki hifadhi za misitu ya Serikali katika wilaya nzima na kibali cha kunyanyasa wananchi, hiyo mikataba ni feki ipitiwe upya, tenda zitangazwe upya na uamuzi wa kuwafukuza ni halali kabisa.