Mmoja wa viongozi wakuu wa uhifadhi wa wanyama pori
barani Afrika Emmanuel de Merode, amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa
risasi na watu wasiojulikana katika moja ya mbuga kongwe barani afrika.
Bwana Merode,ambaye ni raia wa Ubelgiji ni
mkurugenzi wa mbunga ya wanyama pori ya Virunga,ambayo ni makao ya Sokwe
wanaokaa milimani katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Sokwe hao ni baadhi ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka kutokana na kuwindwa sana.
Alipigwa risasi akiwa anaendesha gari kati ya
eneo lililo kati ya makao makuu ya mbuga hiyo na mji wa Goma ambako
amelazwa hospitalini.
Sababu ya kupigwa risasi kwa mhifadhi huyo
haijajulikana, lakini makundi ya watu ambao hukata miti kiharamu,
wawindaji haramu na waasi huendesha shughuli zao katika eneo hilo.