HOTUBA YA KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII BI. TARISHI, M.K. KATIKA UFUNGUZI WA WARSHA YA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI, MWANZA, TAREHE 26 MEI 2014

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Wahariri wa Vyombo vya Habari, Waandishi waandamizi, Mabibi na mabwana, Wageni Waalikwa... thumbnail 1 summary

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Ndugu Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Waandishi waandamizi,
Mabibi na mabwana,
Wageni Waalikwa.
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika warsha hii muhimu ambayo imenipa fursa ya kukutana na Wahariri wa Habari kutoka vyombo mbali mbali hapa nchini. Aidha, napenda kuwapongeza Shirika la Hifadhi za Taifa-TANAPA kwa maandalizi ya Warsha hii. Vilevile nawashukuru nyote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria warsha hii. Mmekubali kuitikia wito kwa nia njema kabisa kwa maendeleo ya nchi na ya sekta ya uhifadhi na utalii.
Ndugu Wanahabari,
Warsha hii ya leo inatuongezea fursa ya kufahamiana na ninyi ambao ni wadau muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Napenda mfahamu kuwa Wizara na TANAPA tunatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika uhifadhi na maendeleo ya utalii nchini. Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuwepo kwa mawasiliano ya karibu baina ya Wizara pamoja na Taasisi zake taasisi na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kufanikisha majukumu yetu. Nimefarijika sana baada ya kufahamishwa kuwa Kauli Mbiu ya Warsha hii ni “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika kukuza utalii nchini”.
Ndugu Wahariri,
Ni wakati muafaka sasa vyombo vya habari viamue kwa makusudi makubwa na kwa kutumia ushawishi mkubwa mlionao kwa jamii kuripoti shughuli za utalii na kuvitangaza vivutio mbali mbali vya utalii vilivyopo hapa nchili ili kuhamasisha watalii wa ndani nje ya nchi. Kazi moja kuu ambayo napenda tushirikiane na vyombo vya habari ni kuongeza ushawishi kwa Watanzania wahamasike na kutalii.
Ndugu Wahariri,
Utalii ni moja ya sekta ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Tanzania. Sekta za Utalii na Madini ndio zinazoongoza katika kuliingizia Taifa fedha za Kigeni. Mwaka 2013 inakadiriwa utalii uliiingiza jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.8 katika uchumi wa nchi. Tafiti zinaonesha kuwa Sekta ya Utalii ilitoa jumla ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zipatazo 1,196,000 katika mwaka 2013. Katika mwaka huo Tanzania ilipokea watalii wa nje wapatao 1,135,884. Wito wetu kama Wizara ni kuwa vyombo vyenu vitumike katika kuzitangaza vema vivutio na hifadhi zetui ili ziweze kutembelewa na wageni wengi zaidi na hatimaye uchumi wa taifa letu uweze kukua kwa haraka zaidi.
Ndugu Wahariri,
Ni matumaini yangu kuwa mtatumia warsha hii kujielimisha kwa undani juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Wizara, hususan za Shirika lake la TANAPA kupitia kwa watoa mada ili muweze kuwa na uelewa mpana katika maeneo haya na hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku.
Baada ya kusema hayo, nashukuru tena kwa kupata fursa hii ya kuongea nanyi na napenda kutamka kwamba warsha hili imefunguliwa rasmi.
Nashukuru sana kwa kunisikiliza
Asanteni