Klabu ya Arsenal imepanga kutuma maofisa biashara wake jijini Dar es
Salaam, Tanzania kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano na
wafanyabiashara kadhaa wakubwa nchini Tanzania.
Huu utakuwa ujumbe wa kwanza kabisa wa Arsenal nchini Tanzania,
ambapo klabu hii kubwa ya England inataka kujenga ushirika mkubwa kabisa
katika maeneo ya masoko na chapa zake, ili kutanua mafanikio
yaliyofikiwa kwenye nchi nyingine za Afrika kama Kenya, Uganda na
Nigeria.
Washika Bunduki hao wa London wanataka kutoa fursa kwa benki za
Tanzania pamoja na kampuni za simu na taasisi nyingine kuweza kupata
rasilimali zihusianazo na Arsenal, kama vile bidhaa zilizosainiwa kwa
majina ya wachezaji, tiketi za mechi.
Safari hii kwa kiasi kikubwa imefanikishwa na Ubalozi wa Tanzania
katika Uingereza, Kupitia kwa Mhe Balozi Peter Kallaghe, ambaye binafsi
ameshiriki kuwaarifu maafisa hao, mazingira ya nyumbani, na ukuaji wa
sekta za binafsi katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Arsenal wanasema kwamba wanaweza kuwapatia washirika wao hao uwanja
mpana wa masoko kwa ajili ya kuwasaidia kutimiza malengo mbalimbali ya
kibiashara.
Ofisa Biashara Mkuu wa Arsenal, Vinai Venkatesham amesema kwamba
wameichagua Tanzania kwa sababu wana washabiki wengi, na kwa
kushirikiana na taasisi za Tanzania, watakuwa karibu zaidi na washabiki
wao kuliko ilivyokuwa awali.
“Katika bara lenye nchi zaidi ya 50, tumechagua kuzuru Tanzania
kimkakati kwa sababu tunaiamini nchi hiyo. Arsenal ina mamilioni ya
Watanzania ambao ni washabiki waaminifu na wenye mapenzi makubwa nayo.
“Kwa kushirikiana na taasisi za huko, tutaweza kuisogeza klabu karibu
zaidi na washabiki hao kuliko ilivyokuwa awali, huku tukizipatia
taasisi husika fursa pekee za kuifikia klabu yetu,” akasema Venkatesham.
Wajumbe hao wa jopo la Maendeleo ya Ushirikiano ya Arsenal
wanatarajia kuwasili nchini Tanzania Januari 18 mwaka huu, ambapo
watakaa kwa wiki moja jijini Dar es Salaam, kuitisha mikutano kadhaa ya
awali ya kibiaashara na kuzindua rasmi mchakato wa kutafuta washirika wa
kwanza kabisa nchini Tanzania.
Chanzo: Tanzaniasports