Dulu za kitafiti
zinaeleza kuwa, Wakulima wa Mkoa wa Morogoro wanakabiliwa na janga
kubwa la ugonjwa wa wa ‘Kimyangu’ ambapo virusi kitaalamu vikijulikana kama (Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) ushambulia mpunga shambani.
Kwa
mujibu wa Afisa Kilimo Bwana. Joseph Nyange katika Wilaya ya Ulanga,
ambaye alifanya mahojiano na mwandishi wa mtandao huu katika Tarafa ya
Mtimbira iliyopo Mkoani Morogoro, anakiri tatizo hilo kwa mwaka huu
limekuwa kubwa hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea
kuikumba Tanzania kila wakati.
Bwana
Nyange anaeleza kuwa, tatizo hilo la virusi vya RYMV ama Kimyangu,
kushambulia mazao ya wakulima katika ukanda huo, ni baada ya mwaka jana
na mwaka huu kutokea mabadiliko ya unyeshaji wa mvua zaidi ya mazoea ya
nyuma.
“Tatizo
hili la ugonjwa wa Kimyangu kwenye mipunga, limeweza kuathiri wakulima
wengi na hali hii imetokea mwaka huu kwa kiwango kikubwa sana. Baada ya
kukosekana mvua ya uhakika iliyosababishwa na tabianchi” anasema Bwana
Nyange.
Anaongeza
kuwa, ugonjwa huo unakuwa mkubwa sana na hasa kipindi ambacho kunakuwa
na jua kali hivyo mashamba mengi yanakumbwa na athari hiyo ya Kimyangu.
Athari hizo zinakuwa kilio kikubwa kwa wakulima kwani hadi sasa
ugonjwa huo haujapatiwa dawa licha ya wataalam kuendelea kufanya
utafiti huku wakulima nao wakiendelea kujaribu kutibu mashamba yao kwa
kutumia madawa ya kienyeji.
Hata
hivyo, Bwana Shamba huyo, ana kili kuwa, kuwa licha ya Ugonjwa huo
kuwa si mgeni sana kwa ukanda huo, Kwa Tanzania upo karibu sehemu
mbalimbali huku tofauti yake ni namna ya uibukaji wake.
“Ugonjwa
huu upo maeneo mbalimbali ya Tanzania hasa sehemu zinazolimwa mpunga
kwa wingi ndani ya Tanzania na hata nje ya Tanzania hasa kwa nchi hizi
za jangwa la Sahara. Kwa kwetu huku mwaka huu tumeathiriwa na mabadiliko
ya tabianchi, kwani kukatika ghafla kwa mvua na kupelekea jua kuwa
kali na athari pia imekuwa kali” anaeleza Bwana Shamba huyo.
Mvua zilivyo athiri
Bwana
Shamba Joseph Nyange anaeleza kuwa, kwa mwaka jana na mwaka huu mvua
zilichelewa na hata zilipokuja zilinyesha kwa kiwango kidogo tofauti na
viwango vya mvua vilivyozoeleka hapo awali. Lakini mvua hiyo hiyo
iliyochelewa kunyesha na hata kuwa kwa kiwango kidogo, ilikatika ghafla
na kusababisha ugonjwa huo kuwa mkubwa huku akibainisha kuwa, kwa mwaka
huu pekee mvua ilikatika ghafla mnamo mwezi wa tano na baada ya hapo
haikunyesha tena hadi sasa.
Hata
hivyo, ametaja vyanzo vinavyopelekea kwa mabadiliko ya tabianchi
katika maeneo hayo ni pamoja na ukataji wa miti hovyo hasa katika vyanzo
vya maji, Kuingia kwa wafugaji wengi katika maeneo ya ardhi yenye
rutuba ya kilimo na upanuzi wa mashamba ambapo watu wengi kwa sasa
wameweza kulima hadi milimani mazao ambayo yanafyonza maji mengi ambapo
shughuli hizo za kibanadamu ndizo zinazopelekea kutotabirika kwa misimu
ya mvua ya uhakika na hata kusababisha ugonjwa huo kuendelea kuwa sugu
katika mazao ya mpunga.
Utafiti
uliofanywa na mwandishi wa mtandao huu, umebaini kuwa, Mkulima mmoja
ana uwezo wa kupata gunia 10 hadi 15, kwa shamba la hekari moja, ambaye
analima kilimo cha kienyeji, Lakini kutokana na ugonjwa huo wa Kimyangu,
wakulima wengi wamevuna katika shamba kama hilo la hekari moja, wapo
waliovuna gunia moja na wapo waliovuna magunia matano na wapo waliokosa
kabisa kwa shamba zima kuathiriwa na ugonjwa.
(Inaelezwa
kuwa endapo Mkulima wa kawaida, atalima mpunga kwa kutumia kilimo cha
kisasa katika shamba la hekari moja, ana uwezo wa kupata magunia 18
hadi 25).
Inaelezwa
kuwa, ugonjwa huo wa Kimyangu, mpunga shambani unakuwa katika hali ya
kubabuka sana, huku ukiuona shambani kwa mbali ukionekana kama upo
salama, lakini ukiuvuna ndipo utagundua kuwa umeathirika na virusi hivyo
vya RYMV.
Mmoja
wa wakulima katika Kijiji cha Mtimbira, Bwana Daraja Daraaja akiwa
pembeni mwa shamba lake huku kwa kiasi kikubwa mpunga ulioungua kutokana
na mabadiliko ya tabianchi na kupelekea ugonjwa wa virusi vya RYMV ama
ugonjwa wa Kimyangu. (Picha na Andrew Chale, modewjiblog).
Mashuhuda
Baadhi
ya wakulima walizungumza na mwandishi wa mtandao huu katika maeneo
kadhaa ya Wilaya za Mahenge, Ulanga na Kilombero wameweka wazi kuwa,
mabadiliko ya tabianchi wamewaathiri kwa kiwango kikubwa huku na
kushindwa la kufanya licha ya kutegemea kilimo kama mtaji wa kujipatia
pesa na chakula.
Hivyo
kwa kutokea ugonjwa huo kwa kiwango kikubwa umewashangaza sana na
kushindwa kutojua la kufanya kwa msimu wa kilimo hapo baadae kwani
kilimo kikuu kwao ni zao la mpunga.
(Kimyanga
ni kwa Kiswahili cha kawaida au Kimyangu kwa lugha ya Kipogolo, ambao
ni kabila kubwa katika maeneo hayo ya Wilaya za Ulanga, Mahenge,
Kilombero na maeneo mengine ndani ya Mkoa huo wa Morogoro).
“Endapo
hakuna ugonjwa huu wa Kimyangu, huko nyuma tumevuna magunia mengi tu
lakini sasa kila mmoja analia hali imekuwa ngumu, wengine tulikopa
vitu na tulitegemea baada ya kuvuna mpunga turejeshe lakini hali imekua
kinyume” anasema Samson Mwenda, Mkazi wa Mahenge.
Kwa
upande wake, William Sijombele mkazi wa Mtimbila anaeleza kuwa, elimu
ndogo ya kutojua baadhi ya mambo ndio inayopelekea tatizo hilo kuwa
kubwa kila mwaka kwani wakulima wengi wamekuwa wakiendeleza shughuli
nyingi mbadala wa kilimo hali inayochangia athari za mabadiliko hayo.
“Utakuta
Mkulima ana jishughulisha na kilimo hapo hapo ana mifugo. Mkulima huyo
huyo anajishughulisha na biashara ikiwemo ya mbao ama uchoaji wa mikaa
hali ambayo anasababisha athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi. Haya
yote hakuna mtu wa kuingilia kati si Serikali si wanakijiji wengi
wanajiona wapo juu ya sheria” anasema Mzee Sijombele.
Kwa
upande wake mkazi wa Wilaya ya Ulanga, kijiji cha Mtimbira, Bwana.
Daniel Nguji anabainisha kuwa, yeye kwenye shamba lake la hekari tano,
alitegea angepata magunia zaidi ya 50, lakini baada ya kutokea ugonjwa
huo wa Kimyangu, ameweza kuambulia magunia machache kiasi cha kupata
athara kubwa.
“Kuliandaa
shamba, upandaji na kuulinda mpunga shambani hadi kufikia hatua ya
kuvuna, inagharimu pesa nyingi sana. Huu ugonjwa wa mpunga umenitia
athara kubwa tunaomba wataalamu watupatie dawa ilikukabiliana na ugonjwa
huu” anaeleza Nguji.
(Kwa
mauzo: Mtimbira Gunia moja la Mpunga wanauza kuanzia kiasi cha
Sh.60,000, hii ikiwa ni gunia la debe Saba, yaani debe moja la Mpunga
likiwa linauzwa kwa Sh. 8000.)