TMA: Kuanzia mwezi Juni hadi Agosti 2016, ni baridi kali na kipupwe nchini

Kuna kipindi fulani hivi, kuanzia miwshoni mwa mwaka jana 2015 hadi mwanzoni mwa mwaka huu 2016, usemi wa 'usiniguse' ulikuwa maa... thumbnail 1 summary
Kuna kipindi fulani hivi, kuanzia miwshoni mwa mwaka jana 2015 hadi mwanzoni mwa mwaka huu 2016, usemi wa 'usiniguse' ulikuwa maarufu sana miongoni mwa wanandoa. Sababu kubwa ikiwa ni joto kali ambalo hakuna aliyetaka kuguswa kwa joto lile lililosababisha watu watokwe na jasho kama wamemwagiwa maji.
Lakini Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekuja na habari njema kwa wanandoa hao ambapo sasa imetabiri kuwapo kwa hali ya baridi na kipupwe katika kipindi cha Juni hadi Agosti, mwaka huu. (Wenye kutafuta watoto kazi kwenu)

 
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha mamlaka hiyo, Samuel Mbuya, anasema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya madhara yanayoweza kuwakumba. 
 
Mbuya anayataja maeneo yatakayokumbwa na vipindi vifupi vya mvua ni ukanda wa Ziwa Victoria na Pwani ya Kaskazini katika visiwa wa Pemba na Unguja.

Anasema katika miezi hiyo, maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa makavu na yenye hali ya baridi kiasi katika maeneo machache kutokana na majira hayo ya kipupwe.

"Utabiri huu unaonyesha pia katika maeneo mengi ya nchi kutakuwa na joto la wastani chini hadi juu ya wastani na izingatiwe kuwa kipindi cha baridi kitakuwa nyakati za usiku na asubuhi," anasema.

Meneja huyo aliyekuwa akizungunza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema hali hiyo inasababishwa na kupungua kwa joto la bahari katika ukanda la bahari, hususan katika ukanda wa Tropiki ya Pacific sambamba na joto bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Mbuya anasema hali hiyo itasababisha upepo kuvuma kutoka magharibi kwenda mashariki, hususan katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa TMA, Monica Mutoni, akawataka wananchi kuchukua tahadhari zilizochukuliwa na mamlaka hiyo kupitia taarifa walizozitoa ili kuokoa maisha na mali.

"Hivi karibuni TMA imekuwa ikitoa tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa upepo mkali na mawimbi makubwa kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi, maziwa na nchi kavu.
Ni vyema wananchi hasa wale watumiaji wa bahari na maziwa kuchukua hatua pindi taarifa kama hizo zinapotolewa," anasema.

Chanzo Nipashe