Kilimo cha mpunga kinavyotishia utajiri wa mikoko Delta ya Rufiji

Hellen Ngoromera   DELTA ya Rufiji ni eneo linalopatikana katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Ofisa Misitu Wizara ya Maliasil... thumbnail 1 summary

Hellen Ngoromera
 
DELTA ya Rufiji ni eneo linalopatikana katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Ofisa Misitu Wizara ya Maliasili na Utalii, Zakaria Kitale, anasema eneo hili ni moja ya maeneo ambayo maji ya baridi kutoka katika maporomoko na mito mbalimbali yanakutana na kuingia katika Bahari ya Hindi.

Anasema maji baridi hayo yanaingia katika Bahari ya Hindi kupitia njia 11 ambazo zinajulikana kama matoleo au mito iliyopewa majina mbalimbali.

“Matoleo hayo ya maji ya Mto Rufiji yana jumla ya eneo la kilomita za Mraba 12,000 ikijumuisha pwani na vijiji kadhaa. Matoleo hayo yana wastani wa urefu wa kilomita 65 na upana wa kilomita 23,” anasema Kitale.

Anaongeza kuwa matoleo hayo ni maarufu kama mto Kikayu, Simbaulanga,Saninga, Kiomboni, Bumba, Mamba, Dima, Mdahu, Ngedu, Jaja na Muhoro na kwamba hiyo ndiyo mito maarufu ambayo kwa pamoja huingiza maji baridi katika Bahari ya Hindi na hivyo kulifanya eneo hilo kuitwa Delta ya Rufiji.

Anasema Delta ya Rufiji ni maarufu sana kwa mikoko ambayo imeshamiri kupindukia, delta hii ina mikoko ya aina nane yenye ukubwa wa hekta 53,000 ambazo ni sawa na nusu ya eneo lote la mikoko inayopatikana Tanzania katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi kutokea kaskazini na kusini mwa Tanzania pwani ya Tanga hadi pwani ya Mtwara na vitongoji vyake.

“Eneo hili la mikoko katika wilaya ya Rufiji lina historia yake hasa ikizingatiwa kuwa eneo hili lilitengwa tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani alipokuwepo nchini,” anasema.

Anaeleza kwamba mikoko katika delta hiyo ilitangazwa kuwa msitu wa hifadhi ya serikali mwaka 1928 na hali hiyo inatokana na umuhimu wa miti hiyo kwa mazingira ya bahari, viumbe wa baharini na nchi kavu.

Kwa mujibu wa Ofisa Misitu huyo mikoko pia hutumika kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika pwani mbalimbali kutokana na kuongezeka kwa maji ya bahari na kwa kulitambua hilo ndio maana wakoloni walilitenga eneo hilo kwa ajili ya kulihifadhi.

Anasema mikoko ina faida nyingi hasa kwa kuhifadhi mazingira na viumbe hai, mikoko ni mazalia ya samaki aina ya Kamba, hutoa nguzo zitumikazo kujengeea, hutoa magogo, magamba yaker hutumika kutengeneza dawa za kulainishia ngozi, hutoa kuni, mkaa hivyo kuongeza pato la taifa.

Anasema mikoko pia huzuia mawimbi ya bahari na kupunguza kasi ya vimbunga, mmomonyoko wa ardhi, upepo mkali kutoka baharini kwenda nchikavu, hukinga matumbawe yasifikiwe na vumbi na udongo kutoka nchi kavu.

“Mikoko pia hurekebisha tabianchi kwa kunyonya hewa chafu, kuchuja sumu baharini na kuhifadhi baianuwai,” anasema mtaalamu huyo wa misitu.

Anasema pamoja na faida zote hizo zitokanazo na mikoko, wakazi wa Delta ya Rufiji, bado hawajaziona faida zake na kwa sasa inakabiliwa na tishio moja kubwa kutoka kwa wananchi hao.

Analitaja tishio hilo kuwa ni kilimo cha mpunga ambacho kinafanywa katika visiwa vingi vinavyopatikana katika delta hiyo na wananchi.

Anasema kilimo hicho ni cha msimu na huanza mwezi Desemba hadi Juni. “Kwa hakika ni kero kubwa kwa mikoko, viumbe hai na mazingira kwa ujumla ambavyo vinapatikana katika pwani hiyo.

Ni kero kwani inabidi mikoko ikatwe na mazingira ambayo mikoko huota iharibiwe na kuua viumbe hai wote kama kaa ili ardhi iwe tayari kwa kilimo cha mpunga,’ anasema Kitale.

Anasema baya zaidi ardhi lazima imwagiwe dawa hatari kwa mazingira na viumbe hai aina ya DDT au Thiodan ndipo iwe tayari kuotesha mpunga kwani alkaline inayopatikana katika ardhi inayootesha mikoko haiwezi kuotesha wala kukuza mpunga kwa hiyo ni lazima itolewe kwanza.

Anasema wananchi hao wanapendelea kulima katika ukanda huo wa mikoko kwa kuwa maeneo hayo ni sehemu ambazo hazijawahi kujishughulisha na kilimo kwa ujumla, mashamba mapya hutoa mazao mengi kwa miaka mitatu hadi minne mfululizo na yana rutuba nyingi na hakuna magugu.

Anasema kilimo cha mpunga kinaathiri mikoko kwani huleta majani na miti ya kigeni katika ardhi ambayo huotesha na kushamirisha mikoko, baada ya kufyeka mikoko ili kupata ardhi ya kilimo cha mpunga.

Anaweka bayana kwamba ujio huo wa miti na majani hayo huifanya ardhi kuwa ngumu na kushindwa kupitisha hewa kama ilivyo kawaida yake na kufanya chumvi chumvi ilinayopatikana katika ardhi hiyo kutoweka na hivyo kufanya kaa kutoweka na mikoko kutoota tena.

Anasema pia majani hayo huletwa na mikondo ya maji ambayo kwa sasa imeshamiri baada ya kuwa imebadili mwelekeo na hivyo kuleta majani hayo ambayo ni magugu, uelekeo wa maji katika delta ya Rufiji unaelezwa kuwepo tangu miaka ya 1970 hali ambayo inaendelea hadi sasa na hivyo kushamirisha kasi ya kilimo cha mpunga.

“Wataalamu wanasema maji badala ya kuelekea mashariki kama ilivyo kawaida yake na kuingia baharini tangu miaka ya 1970 maji yamekuwa yakielekea kaskazini mwa delta hiyo, hali ambayo imekuwa ikiongeza tishio la ustawi wa mikoko katika eneo ambalo ilikuwa imehifadhiwa kwa sehemu kubwa kuliko sehemu nyingine yoyote nchini,” anasema.

Anaeleza kwamba inaelezwa kuwa hali ya kubadili uelekeo wa maji pia imekuwa inachochea kwa kiasi kikubwa vitendo vya wananchi kuingia katika pwani za visiwa mbalimbali vilivyoko katika delta hiyo na kuanza kulima mpunga kwani maji hayo yanapunguza maji ya chumvi ambayo hayaendani na kilimo cha mpunga.

Kwa mujibu wa Kitale kasi hiyo ya kilimo cha mpunga kwa bahati mbaya imewezesha kufikiwa kwa eneo la mikoko ambalo ni zuri kwa ajili ya biashara ya miti ya mikoko lenye ukubwa wa hekta 25,000 hali ambayo inafanya kuwa eneo lililoathiriwa na kilimo hicho katika Delta hiyo kufikia hekta 8,000.

Anasema hali hiyo inatishia uwepo wa mikoko ambayo kwa kiasi kikubwa umekuwa ni utajiri mkubwa katika wilaya hiyo, inapendezesha kwa kiasi kikubwa mandhari ya delta ya Rufiji kwani unaposimama pembezoni mwa mto Rufiji utaona pwani zake zote zikiwa zimesheheni miti ya mikoko ikiwa imeambatana na utulivu mkubwa na wa aina yake.

Anasema kwa kuzingatia hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na Mashirika ya kimataifa na mashirika mbalimbali ya uhifadhi mazingira yamekuwa yakishiriki katika programu mbalimbali za ulinzi na uhifadhi wa miti hii aina ya mikoko ili kuweza kunufaika nayo na kuifanya iendelee kuwepo.

Anasema hayo yamekuwa yakifanyika lakini wakulima hao wamekuwa hawakubaliani na mpango wa kulinda na kuhifadhi mikoko ambao umekuwa ukiwataka wapande mikoko katika maeneo waliyovamia na hata wengine kudiriki kuing’oa mikoko mingine waliyokuta imeoteshwa.

Anaeleza kwamba serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kupitia programu mbalimbali ili kuuelewesha umma kuhusiana na umuhimu wa mikoko kwa mazingira, viumbe hai na kiuchumi kwa ujumla.

“Hili pia linapaswa kuwa jukumu la wananchi wote hasa wale wanaoishi katika maeneo kama ya Delta ya Rufiji ili kuweza kutunza miti hiyo ya mikoko kwa faida ya watu na mazingira kwa ujumla,” anasema Kitale.

Anasema ni jukumu la kila mwananchi kuitunza mikoko ili iweze kuiletea nchi manufaa.

helenpendo@yahoo.com au 0754 886 749