Pinda: Nitazifuta halmashauri zenye ‘mchwa’

na Sitta Tumma, Mwanza   WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema atakuwa tayari kuzifuta halmashauri zitazoonekana kuwa vinara wa kufuja ... thumbnail 1 summary

na Sitta Tumma, Mwanza
 
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema atakuwa tayari kuzifuta halmashauri zitazoonekana kuwa vinara wa kufuja fedha za miradi ya maendeleo.

Pinda alitoa kauli hiyo jijini hapa, wakati alipokuwa akihutubia kilele cha maadhimisho ya nane ya siku ya Serikali za Mitaa, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jana.

Alisema kuwa serikali haiwezi kuvumilia madudu ya ulaji wa fedha za umma, unaofanywa na baadhi ya watumishi wakati madiwani wa halmashauri husika wapo.

Kwamba wakati utafika serikali itaagiza na wananchi wawafukuze madiwani wao kwa kushindwa kusimamia fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali kuu.

”Nataka mwaka kesho CAG asikute madudu ya ufisadi kama alivyokuta hivi sasa. Vinginevyo itatulazimu kusema wananchi wawafukuze madiwani wao, maana wameshindwa kusimamia na kulinda fedha za maendeleo,” alisema Pinda.

Maadhimisho hayo ambayo hata hivyo yalidorora kutokana na kuhudhuriwa na idadi ndogo ya watu, yaliyohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, wenyeviti wote wa halmashauri nchini, wakiongozwa na Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Dk. Didas Masaburi.

Pinda pia aligusia suala la amani ya nchi akisema wapo baadhi ya watu wameanza kuichezea kwa kutoa maneno makali ya kushabikia kuwepo kwa machafuko kama yaliyotokea Libya na Misri, jambo alilodai kuwa serikali haitakubali.

Alisema ni vema ushindani wa kisiasa ukawepo majukwaani na kwamba mtu au mwanasiasa yeyote anayeona machafuko ndiyo mazuri kwa kukomboa nchi, huyo ana matatizo mengi akilini.

Awali, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Dk. Masaburi aliipiga kijembe serikali kwa kusema kwamba imesoma alama za nyakati kisha kukubali kuwapo kwa mchakato wa Katiba mpya hapa nchini.

Masaburi aliipongeza serikali kwa kuongeza posho za madiwani akisema kuwa itaimarisha zaidi utendaji kazi wa viongozi hao wa kisiasa.

Chanzo: Tanzania Daima