GEREZA LAANZISHA MSITU

na Ahmed Makongo, Bunda KATIKA kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazingira, Gereza la Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, limeanzisha ... thumbnail 1 summary

na Ahmed Makongo, Bunda KATIKA kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazingira, Gereza la Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, limeanzisha msitu katika eneo lake ili kutunza mazingira na kupata kuni kwa ajili ya matumizi ya gereza hilo.
Mkuu wa gereza hilo, Mrakibu wa Magereza (ASP) John Tunge, alisema hayo juzi mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Kapteni Honest Ernest Mwanossa, wakati Mwenge huo ulipokwenda kukagua mradi huo.
Alisema, upandaji wa miti katika eneo hilo ulianza Oktoba mwaka 2006 na hadi kufikia Juni mwaka 2010, miti 11,963, ikiwemo mihale 10,691 na albizia 1,272, ilishapandwa kwenye eneo la hekta saba na kwamba mradi mzima umegharimu sh milioni 15.
Alisema, kuwa walipanda miti hiyo kwa ushirikiano na shirika moja lisilo la kiserikali la Village Sharing Agency (VISA) la wilayani Bunda, pamoja na Idara ya Ardhi na Maliasili- kitengo cha misitu cha halmashauri hiyo.
Akifafanua zaidi, alisema kitengo hicho kimehusika kutoa mbegu, viliba na ushauri wa kitaalamu.
“Faida za msitu huu ni pamoja na gereza kukata matawi ambayo hutumika kama kuni za kupikia chakula cha mahabusu na wafungwa, pili msitu ni kivuli kwa viumbe... vile vile unatukinga na upepo,” alisema.
Alibainisha kuwa, msitu huo una ulinzi wa kutosha juu ya majanga ya moto, ikiwa ni pamoja na kuhimizana zaidi kwa ajili ya kupanda miti mingi zaidi ili kufikia malengo yaliyowekwa kitaifa.
Naye Kapteni Mwanossa, aliupongeza uongozi wa gereza hilo, pamoja na Shirika la Visa kwa kubuni mradi huo na alizitaka taasisi nyingine nchini kuiga mfano huo ili kukabiliana na changamoto ya uhifadhi wa mazingira.
Chanzo: Tanzania Daima