na Hellen Ngoromera
KAMPUNI ya usafiri
wa anga ya Precision Air, imetangaza kuongeza safari zake za kila siku kufikia
mara tano kwa siku, kuelekea mkoani Arusha, na kuboresha huduma zake za Mwanza,
kuanzia Agosti 22 mwaka huu.
Kampuni hiyo
imezindua safari mpya kwa ndege ya Boeing 737-300 siku za Jumatano, Ijumaa na
Jumapili kwenda Mwanza, ikiwa ni katika kuboresha safari zake na kukidhi
mahitaji ya wateja wake.
Akizungumza
wakati wa kuzindua safari hizo, Mkurugenzi wa Biashara wa Precision Air,
Patrick Ndekana, alisema kuwa kampuni imeshuhudia ukuaji mkubwa kwa kuongezeka
kwa njia za safari za nje na ndani ya nchi kwa nusu msimu sasa.
“Tumeongeza
safari mpya kwenda Lubumbashi na Lusaka kwa miezi miwili iliyopita na kuongeza
kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kampuni. Tunajivunia kukua kwa kampuni yetu kwa
sasa, tuna njia na vituo 16 hadi sasa na tuna lengo la kuboresha ili kuendelea
kuongoza katika huduma za usafiri wa anga nchini,” alisema.
Ndekana
alifafanua kuwa Precision Air ndio kampuni pekee inayoongoza kwa huduma za
usafirishaji wa anga nchini na kutoa huduma za usafiri katika sehemu mbalimbali
za ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa
kampuni ilikuwa katika malengo ya kuboresha safari za ndani zaidi, na hivyo
imeamua kusitisha huduma za safari kwenda Johannesburg, Afrika Kusini, tangu
kuanzishwa kwake kwa takriban mwaka sasa.
“Tumejipanga
kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya usafi wa anga wa ndani kwanza,” alisema
Ndekana.
Pia alibainisha
kusitishwa kwa safari za Kigoma na Musoma kutokana na sababu za kiusalama
pamoja na kupisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma.
Chanzo: Tanzania Daima