KISIWA CHA SAANANE CHAKUSANYA MILIONI 38.3/-

Na Nathaniel Limu, Mwanza HIFADHI tarajiwa ya Kisiwa cha Saanane iliyopo Mwanza, imekusanya mapato ya zaidi ya Sh milioni 38.3 kati ya... thumbnail 1 summary

Na Nathaniel Limu, Mwanza
HIFADHI tarajiwa ya Kisiwa cha Saanane iliyopo Mwanza, imekusanya mapato ya zaidi ya Sh milioni 38.3 kati ya Januari, mwaka jana na Julai, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Kaimu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Donatus Bayona, wakati akitoa taarifa yake kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliyekuwa katika ziara yake ya kikazi katika Mikoa ya Simiyu na Mwanza.

Alisema mapato hayo yanatokana na tozo zilizolipwa na wageni 5,845, ambao kati yao wageni wa ndani ni 5,600 na wa nje ni 245, waliotembelea hifadhi hiyo.

Alisema hifadhi hiyo ina wanyama pori asilia waliopandikizwa ambao ni pimbi, fisi maji, paka mwitu, mbwa, mijusi, aina mbali mbali za samaki wakiwamo sato na sangara.

“Pia tunao nyoka ikiwa ni pamoja na chatu na aina 70 za ndege ambazo miongoni mwao wapo wahamiaji na wakazi,” alisema Bayona.

Aliwataja wanyama waliopandikizwa kuwa ni swalapala, tumbili, kobe, tumbili weusi wanaopatikana kisiwani hapo peke yake.

Kwa upande wake, Nyalandu, aliutaka uongozi wa hifadhi hiyo kuangalia uwezekano wa kuiboresha zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kujenga hoteli zenye hadhi ya kitalii.

“Pia nawaomba mfanye juhudi za makusudi, kuhakikisha panakuwapo na simba hata wawili katika hifahi hiyo,” alisema Nyalandu.

Aidha, aliwaahidi watumishi wa hifadhi mbalimbali za hapa nchini kuwa juhudi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali za kuboresha maslahi yao na vitendea kazi.
Chanzo: Mtanzania