MIFUGO 782 ILIYOPOKWA KWA WAMASAI YAREJESHWA

Na Eliya Mbonea, Arusha. SERIKALI wilayani Ngorongoro imefanikiwa kurejesha mifugo 782 ya Wamasai, baada ya kuchukuliwa na Wasonjo katika ... thumbnail 1 summary

Na Eliya Mbonea, Arusha.
SERIKALI wilayani Ngorongoro imefanikiwa kurejesha mifugo 782 ya Wamasai, baada ya kuchukuliwa na Wasonjo katika mapigano yaliyotokea hivi karibuni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Lali, alisema tayari wamekusanya mifugo hiyo kutoka kwa vijana wa Kisonjo, waliokuwa wamevamia maboma ya Wamasai.

“Hadi sasa tumefanikiwa kukusanya ng’ombe 417 na mbuzi 365 mifugo yote imekusanywa eneo moja ikisubiria wananchi waliochukulia mifugo yao kwenda kuitambua na kuichukua,” alisema Lali.

Alisema baada ya mifugo hiyo kuchukuliwa Serikali ilifanya juhudi za kuwatuliza Wamasai wasilipize kisasi kwa kwenda kudai mifugo yao kwa nguvu.

“Baada ya wananchi hao kutofautiana tulichokifanya ni kuwasihi wafugaji wa Kimasai wasichukue uamuzi wa kudai kwa nguvu mifugo yao, hivyo vyombo husika vilifanya kazi ya kutafuta mifugo hiyo na kufanikiwa kupata idadi hiyo ya 782.

“Hali imetulia japokuwa hayakuwa mapigano kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari hapo awali. Ila kwa sasa baadhi ya vijana wa Kisonjo walioingia kwenye maboma kuchukua mifugo wamekuwa wakijificha kwa hofu ya kukamatwa,” alisema Lali.

Hata hivyo, alipoulizwa kama hali hiyo inaweza kuharibu mpango wa Sensa ya Watu na Makazi lililoanza jana, alisema hajapokea taarifa zozote zilizoathiri mpango huo.

“Hadi sasa hakuna changamoto zilizojitokeza lakini, jioni tutaanza kutembelea maeneo kadhaa, kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya Sensa,” alisema Lali.
Chanzo: Mtanzania