WANANCHI HANDENI WATAKIWA KUTOHARIBU MAZINGIRA

Na Mwandishi Wetu, Handeni. OFISA Miradi wa Kikundi kinachojishughulisha na shughuli za uhifadhi wa mazingira wilayani Handeni, Mkoa wa Ta... thumbnail 1 summary

Na Mwandishi Wetu, Handeni.
OFISA Miradi wa Kikundi kinachojishughulisha na shughuli za uhifadhi wa mazingira wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga (MTNEG), Mwinyijuma Manyeko, amewataka wakazi wa wilaya hiyo, kutoharibu mazingira ili kuepuka madhara yanayotokea kutokana na uharibifu huo.

Amesema kuwa, matatizo mengi yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi, yamekuwa yakisababishwa na shughuli za kibinadamu na kwamba, ili kukabiliana na mabadiliko hayo, lazima wananchi wasiharibu mazingira.

Manyeko aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa simu, ili kueleza majukumu yanayofanywa na kikundi chake.

“Kikundi chetu kinaitwa Mkata Tree Nursery and Envirocare Group na tuliamua kukianzisha baada ya kuona wananchi wanaharibu mazingira bila kujua madhara ya uharibufu huo.

“Tulipoona hivyo, tukaamua kuanzisha kikundi hiki ambapo tunafanya kazi kwa kushirikiana na wananchi kwa kuwaelimisha madhara ya kukata miti ovyo, kuchoma moto mashamba yao au misitu, kuvuna mbao na kufuga mifugo mingi bila sababu za msingi,” alisema Manyeko.

Kwa mujibu wa Manyeko, maeneo yanayolengwa zaidi katika shughuli za kikundi hicho na ambayo yameharibiwa zaidi na wananchi ni Mkata, Magamba, Kimamba na Megelo katika Jimbo la Kilindi.

“Hayo ndiyo maeneo yaliyoharibiwa zaidi ingawa kuna maeneo mengine ambayo yanahitaji huduma zetu na tutahakikisha uoto wa asili, ambao ulikuwa ukisifiwa na kila mtu, unarejea baada ya wananchi kusitisha uharibifu huo wa mazingira,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho, Rajabu Diwani, alisema kikundi chao kina wanachama zaidi ya 100 na kwamba wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea.

“Unajua ndugu mwandishi, mwanzo ni mgumu siku zote kwa sababu sisi kazi zetu ni za kujitolea na tunalo jukumu la kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya baadhi ya kazi wanazozifanya.

“Kwa hiyo, ugumu wa kazi unakuja pale unapomwambia mwananchi asifanye baadhi ya mambo, kwa sababu akiyafanya kutatokea madhara fulani na wakati unamwambia hivyo, yeye anaamini mambo anayoyafanya ndiyo njia ya mkato ya maisha yake.

“Pamoja na hayo, tunajitahidi kadiri tunavyoweza kuhakikisha tunafanikiwa, huku tukiendelea kutafuta wafadhili wa kutuunga mkono katika jitihada zetu hizi,” alisema Diwani.
Chanzo: Mtanzania