Mwenyekiti wa Shirikisho la Utalii Tanzania TCT, Gaudence Temu
Na Idd Uwesu, Arusha yetu
Watanzania wametakiwa kuyapigia kura
maeneo matatu ya asili ambayo ni moja ya vivutio vikuu vya utalii hapa
nchini ili yaweze kushinda na kuwa moja ya maajabu saba ya dunia.
Maeneo
hayo ambayo ni Mlima wa Kilimanjiro, Kasoko ya Ngorongoro maarufu kama
ngorongoro Crater na Hifadhi ya wanyama ya Serengeti.
Rai
hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Utalii Tanzania TCT,
Gaudence Temu wakati wa uzinduzi wa ndege mpya aina ya Boeng 787 ya
shirika la ndege la Ethiopia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Kilimanjaro.
Mwenyekiti
huyo wa Shirikisho la Utalii nchini amesema ni fursa muhimu kwa
watanzania wote kushiriki upigaji kura huo ili kuyawezesha maeneo hayo
muhimu katika uchumi wa nchi kushinda mashindano hayo yatakayosaidia
kutangaza nchi yetu na vivutio vya utalii vilivyopo.
Akirejea Kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Khamis
Kagasheki, alioutoa wakati akiwasilisha Bungeni Bajeti ya Wizara ya
Maliasili na Utalii ya mwaka 2012/13, kuhusu Watanzania kushiriki
ipasavyo kwa kupiga kura kwa njia ya elektronik kwenye shindano la
‘Seven natural wonders, Temu amesema huu ndio wakati muafaka kwa
watanzania wote kufanya hivyo.
Akizungumzia
ujio wa ndege hiyo ya Boeng 787, Temu amesema ni nafasi nyingine kwa
Tanzania kuzidi kupanua wigo wa sekta za usafiri wa anga na utalii hasa
kwa kanda ya kaskazini na kuongeza kuwa anapongeza shirika la Ndege la
Ethiopia kwa kutoa nafasi kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Kilimanjaro kuwa wa kwanza kutumiwa na ndege hiyo kubwa yenye uwezo wa
kubeba abiria wapatao 270.
Amesema
ujio wa ndege kubwa kama hiyo ya boeng 787 kutarahisha ujio wa watalii
kutoka nje ya nchi na kuongeza idadi ya watoa huduma za usafiri wa nga
ambao ni kichocheo kikubwa katika kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Picha za vivutio vinavyopigiwa kura ili viwe miongoni mwa maajabu saba ya dunia
Chanzo: Arusha yetu