Mkokoteni unaovutwa na Punda
WIZARA ya Nishati na Madini imegundua
‘madudu’ katika sekta ya madini, ikiwamo utoroshaji wa madini ya
tanzanite kwa punda na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na kampuni za
migodi nchini.
Kutokana na hilo, imefanya marekebisho
ya mifumo ya ulipaji kodi iliyowezesha kulipwa kwa baadhi ya madeni na
imetangaza Mtanzania yeyote, ikiwamo mfanyakazi wa mgodi atakayetoa
taarifa za utoroshaji wa madini, atapewa asilimia 30 ya thamani ya mzigo
utakaokuwa umetoroshwa.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Stephen Masele alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza katika
uzinduzi wa Kitabu cha Ripoti inayohusu Haki za Binadamu katika Kazi,
Biashara, Mazingira, Ardhi, Ulinzi na Haki ya Mlaji.
Hafla hiyo iliandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na yeye alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa ripoti
hiyo iliyoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi katika kampuni
za madini nchini na uharibifu wa mazingira uliobainika, Masele
alikubaliana nayo na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na
kadhia hiyo.
“Kuna ‘madudu’ mengi na makubwa
yanafanyika, rasilimali za nchi hii zinatoroshwa na kuyeyuka, tumegundua
kule Manyara madini pekee yanayopatikana Tanzania tu ulimwenguni
kote-tanzanite yanatoroshwa kwa punda, hii haiwezekani kukaa kimya, wezi
wa mali zetu ni Watanzania wenyewe, tubadilike,” alisema Masele na
kuongeza: “Kuna watu wanapewa asilimia 10 ya madini yanayotoroshwa,
tumegundua hilo pia sasa tumesema mwananchi au mfanyakazi atakayegundua
utoroshaji na kutoa taarifa kwetu, tutampa asilimia 30 ya fedha ambayo
ni thamani ya mali aliyookoa”.
Akisisitiza ukwepaji kodi, alisema:
“Tena nitoe onyo kwa kampuni zinazokwepa kodi na kukiuka haki za
binadamu hasa katika sekta inayosimamiwa na wizara yetu, waache mara
moja maana kuna mapinduzi makubwa yanafanyika sasa na hatutasita
kuyafutia leseni mara moja”.
Masele alisema walibaini kampuni zote za
madini nchini zikikwepa baadhi ya kodi kupitia uandikaji wa nyaraka zao
na sasa wamezibaini na kuanza kulipa madeni hayo.
Alitoa mfano kampuni ya Barrick katika
ukokotoaji wa hesabu, ilibainika kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni 5.6
na hadi sasa imelipa Sh bilioni 2.3; nyingine ni TanzaniteOne
inayodaiwa zaidi ya dola za Marekani milioni 2.5.
“Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM)
ilikuwa inadaiwa zaidi ya dola milioni 1.4 ambazo sasa imeanza kuilipa
Halmashauri ya Geita, niseme tu kuna mapinduzi makubwa na tunaamini
Watanzania wako nyuma yetu hatuogopi,” alisema Masele.
Kuhusu TanzaniteOne, alisema leseni yake
imekwisha tangu Agosti na Serikali imesitisha kuipa leseni nyingine
mpaka mpango wa kurejesha asilimia 50 ya hisa serikalini ili kuondoa
umiliki binafsi uliopo sasa na masuala mengine ya utendaji vitakapokaa
vizuri.
Alisema katika kuhakikisha kuna
usimamizi mzuri wa kodi na rasilimali za madini, mafuta na gesi nchini,
Wizara inafanya mapinduzi makubwa katika taasisi zake kwa kufumua Bodi,
kupanga mifumo na kuongeza nguvu ya kiutendaji ya rasilimali watu.
Masele alisema miongoni mwa Bodi
zitakazofumuliwa ni pamoja na ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico)
ili kuongeza usimamizi katika sekta ya madini, pia itafanya marekebisho
makubwa ya utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la
Maendeleo ya Mafuta (TPDC).
Alisema lengo la wizara ni kutekeleza
malengo ya kiuchumi ya mwaka 2020 hadi 2025 ya nchi kuwa katika uchumi
wa kati kwa kutumia rasilimali zake hasa madini, gesi na mafuta na
kusisitiza kuwa hawataacha kuwachukulia hatua wezi wa rasilimali,
waharibifu wa mazingira na ardhi.
Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia
wanaharakati wa haki za binadamu, kwamba Serikali inawatambua na
haipingi kukosolewa, lakini kwenye pongezi ipewe, huku akiwahakikishia
kuwa utafiti wao ni moja ya zana za kuendeleza utendaji unaoendelea hivi
sasa katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen
Kijo-Bisimba aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini
kwa kuonesha matumaini mapya kwa wananchi, hasa usalama wao katika
maeneo ya kazi kwenye migodi na kampuni za uwekezaji.
Kuhusu ripoti ya utafiti, Kijo- Bisimba
alisema utafiti ulifanyika nchi nzima na kugundua ukiukwaji mkubwa wa
haki za binadamu kwa wafanyakazi wa migodini, ujira mdogo na usalama
kazini, uharibifu wa mazingira na ardhi.
“Ilizoeleka katika nchi nyingi, kwamba
walaumiwa wa ukiukaji wa haki za binadamu ni Dola, lakini sasa hali hiyo
imebadilika, sekta binafsi inashiriki katika ukiukaji wa haki za
binadamu kupitia mifumo yao ya utendaji na kukwepa kulipa kodi,” alisema
Dk Kijo-Bisimba.
Akitoa takwimu, Wakili na Mratibu wa
Uwajibikaji wa Kampuni na Mazingira wa LHRC, Flaviana Charles alisema
wafanyakazi asilimia 15.77 waliohojiwa walikiri kuwapo na ukiukwaji wa
haki za binadamu migodini na ujira mdogo, hakuna haki ya kujumuika (kuwa
na vyama vya wafanyakazi).
“Pia asilimia 28.22 ya kampuni hazina
sera ya kuzuia ajira kwa watoto na asilimia 4.62 ya kampuni
hazishirikishi wananchi kuchukua ardhi ya uwekezaji, pia watu hawajui
haki zao wanapouziwa bidhaa bandia,” alisema Charles.
LHRC waliiomba Serikali kuhakikisha pia
kuwa familia 20 zinazoishi katika mahema Geita zilizopisha mradi wa GGM,
zinajengewa nyumba. Naibu Waziri Masele alisema tayari GGM imekubali
kujenga nyumba hizo.
Kwa mujibu wa LHRC, utafiti huo ni wa
kwanza wao kuufanya nchini kuhusu masuala ya haki za wafanyakazi, mlaji,
ardhi, mazingira na ulinzi.