HIFADHI ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA)
imeanzisha utalii wa kuona wanyama nyakati za usiku baada ya kupata kibali cha
kufanya hivyo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa nchini TANAPA.
Hifadhi ya Ruaha inakuwa hifadhi ya
tatu nchini kuwa na utalii wa aina hiyo wa kuona wanyama wanaopatikana zaidi
usiku baada ya hifadhi zingine za Manyara na Tarangile.
Wakiwa kwenye magari maalum na kwa
kutumia taa maluum zisizoumiza macho kwa wanyama,watalii watakaofanya utalii
huo wa usiku watapata fursa ya kuona wanyama ambao wanapatikana zaidi usiku
ambapo Mhifadhi Mkuu wa RUNAPA, Bw.Stephano Qolli amewataka watanzania na
walionje ya Tanzania kufika Ruaha na kuona uhalisia wa hifadhi hiyo nyakati za
usiku.
Naye Mratibu wa Mradi wa kuimarisha
maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania,Bw.Godwell ole Meing'ataki na Afisa
Utalii Mwandamizi wa hifadhi ya Ruaha,Bi.Eva Pwelle wamesema kuzinduliwa kwa
shughuli hiyo ya utalii wa usiku ni moja ya mikakati ya kuboresha huduma katika
hifadhi hiyo na kuongeza mapato serikalini.
Mbali na utalii huo wa usiku na vivutio
vingine vinavyopatikana Ruaha,hifadhi hiyo pia inacho kivutio cha Msitu mnene
wa miyombo ukanda ambao watalii huutumia zaidi kwa utalii wa kutembea masafa
marefu na mafupi.
Utalii huo wa kuona wanyama usiku
umeanzishwa miezi miwili iliyipota na kwamba kulingana na Hifadhi ya Taifa ya
Ruaha kugawanyika sehemu mbili za ukanda wa Savana na ukanda wa Miyombo,
inabaki kuwa hifadhi pekee nchini yenye wanyama na ndege wengi
tofautitofauti.