UKUTA CORAL BEACH HATARANI KUBOMOLEWA

na Betty Kangonga UKUTA wa hoteli ya Coral Beach uliopo ufukweni mwa bahari ya Hindi huenda ukabomolewa iwapo utaonekana kukiuka masharti ... thumbnail 1 summary
na Betty Kangonga
UKUTA wa hoteli ya Coral Beach uliopo ufukweni mwa bahari ya Hindi huenda ukabomolewa iwapo utaonekana kukiuka masharti yaliyotakiwa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Robert Ntakamulenga, alisema mwanzoni walisimamisha ujenzi wa ukuta huo kutokana na kutokuwa na vigezo.
Dk. Ntakamulenga, alisema walimshauri mmiliki wa hoteli hiyo kutafuta mkandarasi mshauri, ili kuhakikisha anafanya ujenzi wa ukuta huo ulio na matundu kuwezesha maji kuweza kuingia na kurudi.
Alisema wanalazimika kutembelea eneo hilo leo, ili kuhakikisha masharti ya ujenzi yamefutwa ikiwa ni pamoja na kutakiwa kujenga kwa urefu wa mita moja na upana mita moja.
Mkurugenzi huyo, alisema kuwa iwapo mmiliki huyo atakuwa amekiuka masharti hayo NEMC watalazimika kubomoa ukuta huo ambao unahatarisha mazingira ya viumbe wa bahari.
“Tuliwahi kutembelea katika eneo hilo baada ya kupokea malalamiko…tukamtaka asimamishe ujenzi huo hadi pale atakapopata mkandarasi mshauri,” alisema.
Naye Mwanasheria wa NEMC, Manchare Suguta, alisema NEMC wanafanyakazi kwa kufuata utaratibu wa kisheria unaotakiwa kitaalamu, hivyo hakuna uonevu wowote utakaofanywa.
Chanzo: Tanzania Daima