Kuna madhara mengi
yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo jambo la kwanza ni ongezeko la
joto duniani, hii ni kuongezeka kwa joto katika uso wa dunia.
Mabadiliko ya
tabianchi yameongeza sana mioto ya porini, joto kali, ukame wa kutisha na hata
kupoteza maisha ya binadamu na viumbe hai.
Madhara mengine ni kuongezeka
kwa kina cha bahari mfano mzuri ni katika kijiji cha Gezaulole katika Manispaa
ya Temeke ambapo maji yamechukua sehemu kubwa ya kijiji hicho, pia kuna mifano
mingi sana kama huu katika fukwe mbalimbali za bahari hapa nchini.
Madhara mengine ni
kubadilika kwa misimu ambapo sasa imekuwa ni kitu cha kawaida kuona mvua kubwa
ikinyesha wakati wa kiangazi na wakati wa masika kukosa mvua jambo ambalo husababisha
mafuriko na ukame mkubwa unaoathiri mfumo wa kilimo nchini.
Kuonea kwa jangwa pia
ni moja ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi mfano mzuri ni mikoa ya Dodoma,
Singida na Shinyanga iko katika hatari ya kugeuka jangwa kutokana na kuwepo kwa
ukame mkubwa sambamba na uharibifu wa mazingira unafanywa na wakazi wa maeneo
hayo.
Madhara mengine ni
kuongezeka kwa magonjwa hasa kwa Tanzania ni ugonjwa hatari wa malaria ambapo
katika mikoa kama Kilimajaro na Iringa ambazo zilitajwa kuwa na kiwango kidogo
cha wagonjwa wa malaria katika miaka ya nyuma lakini sasa kutokana na
kuongezeka kwa joto duniani watu wanaougua malaria wameongezeka.
Pia mabadiliko ya tabia nchi yamepunguza pato la taifa hasa
kutokana na kuathiri sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia pato
la taifa na kukuza maendeleo kwa ujumla.
Hata hivyo hatujachelewa katika katika kuinusuru Tanzania
yetu na dunia kwa ujumla kwani kuna kitu tunaweza kufanya, soma makala ijayo
itaeleza njia za kupambana ama kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambazo
kila mmoja wetu kwa nafasi yake anaweza kuzichukua kunusuru maisha ya kizazi
cha sasa na cha baadae.