na Julieth Mkireri, Bagamoyo
MWENYEKITI wa baraza la mji mdogo wa Bagamoyo, Abdullzahoro Sharifu,
ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA)
kuondoa kizuizi kilichopo katika Kijiji cha Gama, Kata ya Magomeni
wilayani humo kwani kimekuwa kero kwa wananchi.
Sharifu alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea na kuzungumza na
wakazi wa Kitongoji cha Gama akisema pamoja na lengo zuri la TANAPA,
lakini kizuizi hicho kimegeuka kuwa kero kwa wakazi hao.
Alisema kwamba kero hiyo si kwa wakazi wa Kitongoji cha Gama pekee
bali na vitongoji jirani na Kijiji cha Matipwili, kwani wakazi hao
wamewekewa muda wa kupita katika kizuizi hicho bila ya kujali shughuli
za wakazi hao wanazofanya.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,
Shukuru Mbato, amekiri kuwapo kwa kero hiyo ambayo imekuwa ikiwakwamisha
wakazi wa vijiji hivyo kufanya shughuli zao za maendeleo kwa muda
wanaotaka.
Mbato alisema kutokana na hali hiyo anatarajia kumuomba Mkuu wa Wilaya
hiyo, Ahmed Kipozi, kuongozana na wajumbe wa baraza la madiwani na wale
wa mji mdogo kwenda kuzungumza na uongozi wa TANAPA na wakazi wa
vitongoji hivyo ili suala hilo liweze kupatiwa ufumbuzi na kuondoa kero
iliyopo kwa wananchi.
Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com