Kibali cha kuuza meno ya Tembo chasitishwa

na Asha Bani WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesitisha maombi ya kibali cha kuuza meno ya tembo ili ipate muda wa kutosha wa kutekel... thumbnail 1 summary
na Asha Bani
WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesitisha maombi ya kibali cha kuuza meno ya tembo ili ipate muda wa kutosha wa kutekeleza masharti yaliyotolewa na CITES ambayo yanatakiwa yatimizwe kama kigezo cha kuruhusiwa kuuza.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, George Matiko, ilisema kuwa awali wizara ilipeleka maombi CITES ya kutaka kuuza jumla ya tani 101 za meno hayo na kwamba ili kufanikisha hilo ikaomba tembo wa Tanzania washushwe kutoka daraja la kwanza la CITES kwenda daraja la pili ili uuzaji uweze kufanyika kwa taratibu za CITES.
Matiko alieleza kuwa CITES ilitoa vigezo mbalimbali ambavyo hata hivyo vinahitaji muda wa kutosha wa kuvitekeleza.
Aliviainisha vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kudhibiti ujangili wa tembo nchini na kudhibiti meno yanayopitishwa kutoka nchi jirani, kufanya sensa upya ili kupata takwimu mpya za idadi ya tembo walioko nchini na kuboresha upya data (database) ya meno hayo.
Matiko aliongeza kuwa ili kutekeleza vigezo hivyo ipasavyo, wizara imeamua kusitisha ombi lake la kuuza meno ya tembo, ambalo lingejadiliwa kwenye mkutano wa 16 wa CITES utakaofanyika Bangkok Thailand mwezi Machi 2013.
“Ombi la kuuza meno ya tembo litapelekwa tena kwenye mkutano wa 17 wa CITES utakaofuatia ule wa Bangkok; bado Tanzania ambayo ina nia ya kuuza shehena ya meno hayo iliyoko nchini ili kujipatia fedha za kuendeleza uhifadhi,” alisema.
Meno yatakayouzwa ni yale yaliyotokana na tembo waliozeeka na kufa vifo vya asili na waliouawa baada ya kutishia maisha ya binadamu na mali zao.

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com