Majangili wa kigeni watanda nchini, waua tembo zaidi ya 80 Ruaha, Serengeti

MAJANGILI wanaodaiwa kutoka nchi za Rwanda na Burundi, wameingia nchini na kuendesha ujangili katika hifadhi ya taifa ya Ruaha na kuua ... thumbnail 1 summary

MAJANGILI wanaodaiwa kutoka nchi za Rwanda na Burundi, wameingia nchini na kuendesha ujangili katika hifadhi ya taifa ya Ruaha na kuua tembo zaidi ya 80 katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Wakati hali ikiwa hivyo Ruaha, watuhumiwa wanne raia wa kigeni kutoka nchi jirani wameuawa na askari katika hifadhi ya Serengeti na kukutwa na silaha kali za kivita.
Katika matukio ya Ruaha, majangili hao wakiwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG, Shot Gun, 404, 3006 na Trap Gun, wameendesha ujangili kwa kuwatumia wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo inayozungukwa na mikoa ya Dodoma, Mbeya na Iringa.
Akizungumza na wandishi wa habari juzi katika makao makuu ya hifadhi hiyo, Kaimu Mhifadhi wa Idara ya Ulinzi, Edmund Murashani, alisema kuwa ujangili umeshamiri kutokana na idadi ndogo ya askari katika hifadhi hiyo.
Alisema kuwa majangili hayo yamekuwa yakijificha kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi kwa magari ya doria huku hifadhi za kijamii zikishindwa kukabiliana na ujagili huo kutokana na kuwa na silaha duni.
Murashani aliongeza kuwa wanyama wanaoongoza kuuawa ni tembo, twiga, tandala, nyati na wengine wadogo wakiwamo swala, huku adhabu ndogo zinazotolewa kwa wakosaji zikidaiwa kuwa ni kikwazo katika mapambano dhidi ya ujangili.
Pamoja na kukiri kuwa silaha hizo za kivita zinatoka katika nchi hizo, alisema wengi wa wanaokamatwa ni wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wagumu kutaja mtandao unaowafadhili.
Alifafanua kuwa, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani pamoja na watuhumiwa kuachiliwa kwa kile kinachodaiwa kukosekana kwa ushahidi wa kuwatia hatiani ni moja ya changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo katika kukabiliana na ujangili.
Murashani alisema kwa upande wa Dodoma majangili kutoka Rwanda huingilia Wilaya ya Chamwino na kupolekewa na wenyeji ambao zamani walikuwa wakitumia upinde katika kuua wanyama, lakini kwa sasa wamekuwa wakikamatwa na silaha nzito za kivita ambazo huingizwa na majangili hao kutoka nchi jirani.
Naye Ofisa Uhusiano mwandamizi wa Tanapa, Catherine Mbena, alisema ni vigumu kuuhusisha mtandao wa ujangili na wafanyabiashara wakubwa kwa vile hadi sasa hakuna kigogo yeyote aliyekamatwa.
Wanne wauawa Simiyu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Salumu Msangi alisema watuhumiwa hao wanne ambao majina yao hayakufahamika wanakadiriwa kuwa na umri kati ya mika 25 na 40, na kwamba walikutwa ndani ya hifadhi ya Serengeti.
Alisema kuwa Januari 22 mwaka huu, saa 11:30 jioni katika eneo la Mlima Ngoma ndani ya hifadhi hiyo, askari wa wanyamapori wa doria walisikia milio ya risasi mfululizo na walipofuatalitia ghafla walishambuliwa kwa risasi mfululizo kutoka eneo hilo.
Katika majibizano hayo, majangili wanne waliuawa na bunduki aina ya SMG isiyo na namba, risasi 367 za SMG na SAR, magazine saba za SMG, maganda 55 ya SMG, shoka moja, mapanga wawili na visu viwili vilikamatwa.
Kamanda alifafanua kuwa pia walikuta tembo mkubwa akiwa ameuawa, huku pembe zake zikiwa zimeondolewa lakini walizipata na kuzihifadhi.
Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka 2012 jumla ya tembo 10 wameuawa ndani ya hifadhi hiyo na kundi la majangili linalosadikiwa kutoka nchi jirani wakishirikiana na baadhi ya wazalendo.
Majangili hao wanasadikiwa kula njama na baadhi ya wananchi wa vijiji vya Logalombogo, Mwamongo, Mwasengela, Matale, Buruti, Sakasaka katika ukanda wa Wilaya ya Meatu inayopakana na hifadhi za pori la akiba la Maswa na Ngorongoro.

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com