Serengeti yashinda tuzo ya kimataifa

na Asha Bani HIFADHI ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa mwaka 2013. Meneja... thumbnail 1 summary


na Asha Bani
HIFADHI ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa mwaka 2013.
Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi la Taifa nchini (TANAPA), Paschal Shelutete imesema katika taarifa yake kuwa ushindi huo umekuja baada ya Serengeti kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji wa tuzo, na hivyo sasa itapokea tuzo hiyo katika hafla maalumu itakayofanyika mjini Madrid nchini Hispania leo.
“Tuzo hizi huandaliwa na taasisi maarufu duniani inayofahamika kama Global Trade Leaders’ Club inayohusisha makampuni yapatayo 7,000 duniani na ilianzishwa kwa ajili ya kutambua na kuenzi michango inayotolewa na taasisi na makampuni yanayojihusisha na utalii, hoteli pamoja na huduma za vyakula kama njia ya kuthamini mchango na kuhamasisha wale wote wanaofanya kazi katika sekta hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi husika.
“Hifadhi ya Serengeti ni kongwe nchini iliyoanzishwa miaka zaidi ya 50 iliyopita ambayo pia ni eneo la urithi wa dunia na ni maarufu kwa nyumbu wahamao kila mwaka katika mzunguko unaohusisha nchi mbili za Tanzania na Kenya,” alisema Shelutete.
Alisema kutolewa kwa tuzo hiyo ni heshima kwa TANAPA na nchi kwa ujumla, na ni matokeo ya sera nzuri za uhifadhi zinazosimamiwa na TANAPA katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyotengwa kisheria kama hifadhi za taifa yanaendelea kuhifadhiwa vema kwa ajili ya vizazi vijavyo.


Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com