10 waingia fainali Miss Utalii 2013

WAREMBO 10 wamefuzu kuingia fainali ya shindano la Miss Utalii Tanzania mwaka 2012/2013 iliyopangwa kufanyika mwisho wa mwezi huu katika... thumbnail 1 summary


WAREMBO 10 wamefuzu kuingia fainali ya shindano la Miss Utalii Tanzania mwaka 2012/2013 iliyopangwa kufanyika mwisho wa mwezi huu katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagara, jijini Dar es Salaam.

Hao wametokana na warembo 40 ambao juzi walichuana katika Ukumbi wa Msasani Beach katika hatua ya nusu fainali ya shindano kupitia kigezo cha vipaji ambapo 30 walichujwa na kubaki idadi hiyo.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Rais wa Kamati ya Miss Utalii Tanzania, Gideon Chipungahelo, alisema vigezo vilivyotumika kuwachuja warembo hao ni vipaji ambapo kila mshiriki alitakiwa kucheza ngoma ya asili yake.

“Kila mshiriki ameweza kuonesha kipaji chake na majaji wametenda haki katika hili, warembo waliobaki wameonesha vipaji vya hali ya juu,” alisema.
Chipungahelo aliwataja warembo hao na mkoa waliotoka kwenye mabano ni Furaha Kinyunyu (Ruvuma), Marry Lita (Manyara), Joan John (Lindi), Irene Richard wa Chuo Kikuu cha St. Joseph cha Dodoma.
Wengine ni Nadia Marijebi (Zanzibar), Sophia Yussuph (Dar es Salaam), Magreth Malalle (Tabora), Zena Ally (Kigoma), Erica Elibariki (Dodoma) na Asha Ramadhan (Katavi).
Naye Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, aliyekuwa mgeni rasmi, aliwatakia maandalizi mema washiriki wote ambao wamefuzu kushiriki fainali.

“Shindano bado linaendelea sina mengi ya kuongea ila naomba shindano hili litumike kuelimisha watalii na Watanzania wote kujifunza kitu cha asili yetu,” alisema Azan.

Mwaka huu shindano hilo linafanyika chini ya udhamini wa kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-cola Kwanza Ltd, Daja Salon, Mtwana Catering Services Enterprises, Zizzou Fashion, Global Publishers, Ikondolelo Lodge, Clouds Media Group, Tone Multimedia Group na Valley Spring.

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com Do you have any news about aviation services, environmental issues, natural resource and tourism? please do send it to kingkahindi@gmail.com