Viwanja vya ndege katika migodi havina athari

na Sitta Tumma, Mwanza IDARA ya Madini imeeleza kwamba kitendo cha wawekezaji wa madini kujenga viwanja vyao vya ndege katika maeneo y... thumbnail 1 summary

na Sitta Tumma, Mwanza
IDARA ya Madini imeeleza kwamba kitendo cha wawekezaji wa madini kujenga viwanja vyao vya ndege katika maeneo ya migodini havina athari zozote kwa taifa.
Idara hiyo ilieleza kuwa viwanja hivyo vinasaidia usalama wa madini ikiwa ni pamoja na kudhibiti uvamizi punde dhahabu au almasi inapotakiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishna wa Madini Kanda ya Ziwa, Salim Salim, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua semina ya masuala ya madini jijini Mwanza, Salim, alikiri kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu uwepo wa viwanja hivyo na kueleza kuwa havitumiki kutorosha dhahabu au almasi kama inavyodhaniwa.
“Kuwapo viwanja vya ndege maeneo ya migodi hakuna tatizo lolote, viwanja hivi vinasaidia sana usalama wa dhahabu na kuepusha uhalifu unaoweza kujitokeza njiani wakati madini yakisafirishwa umbali mrefu hadi kwenye viwanja vikubwa vya ndege,” alisema.
Alisema kwamba, dhahabu au almasi inayosafirishwa kwenye viwanja hivyo inakaguliwa na kuhakikiwa uzito wake na maofisa wa madini waliopo eneo husika, ikiwemo Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Kuhusu maofisa madini kukaa kwa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi, alisema kwamba serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imeweka mkakati maalumu wa kuwahamisha maofisa hao kutoka kituo kimoja kwenda kingine ndani ya mwaka mmoja.

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com Do you have any news about aviation services, environmental issues, natural resource and tourism? please do send it to kingkahindi@gmail.com