Fastjet yatangaza tarehe ya kuanza kwa safari zake kati ya Dar-Johanesburg

Shirika la ndege lenye bei nafuu, Fastjet limetangaza kuwa safari yake ya kwanza ya kimataifa kati ya Dar es Salaam na Johennesburg itaanza ... thumbnail 1 summary
Shirika la ndege lenye bei nafuu, Fastjet limetangaza kuwa safari yake ya kwanza ya kimataifa kati ya Dar es Salaam na Johennesburg itaanza rasmi Septemba 27 mwaka huu.

Afisa Biashara Mkuu wa fastjet Richard Bordin, ameeleza kuwa uhaba wa safari za ndege kati ya Dar es Salaam na Johannesburg unaotokana na kuwepo kwa shirika moja la ndege na kukosekana kwa ushindani kumesababisha kupanda kwa bei za nauli na kwamba fastjet itaziba pengo hilo.

“Kuanza kwa safari zetu kutapunguza gharama hizo za ndege na kuongeza kasi ya wafanyabiashara na watu wa kawaida kusafiri kati ya Dar es Salaam na Johannesburg kwa shughuli mbalimbali kwa bei nafuu” anasema Bordin

Ikitumia ndege aina ya Airbus A319, fastjet itafanya safari zake mara tatu kwa wiki na huenda idadi ya ‘ruti’ hizo ikaongezeka katika siku za usoni kutegemea na wingi wa wasafiri.

Taarifa zaidi zinasema kuwa tiketi za safari kati ya Dar es Salaam na Johannesburg zitaanza kuuzwa siku ya Jumatano tarehe 31 Julai mwaka huu ambapo nauli ya chini ni dola 100 za kimarekani sawa na sh. 160,000 za kitanzania.