UMOJA wa Waongoza Watalii Tanzania (TATO),
wameiomba serikali kushirikiana nao kikamilifu kukuza sekta ya utalii hapa
nchini ili kuongeza mapato ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa TATO, Wilbard
Chambulo, alipokuwa akijibu hoja za wabunge mbalimbali waliohudhuria semina
iliyoandaliwa na umoja huo kwa lengo la kuwaelimisha umuhimu wa sekta ya
utalii.
Chambulo alisema Kenya inapiga hatua kubwa katika
kutangaza utalii, kuongeza watalii, kurekebisha sheria na kukarabati
miundombinu kutokana na serikali ya nchi hiyo kushirikiana na sekta binafsi
zinazojishughulisha na masuala ya utalii.
Alisema kama Serikali ya Tanzania haitabadili dhana
yake dhidi ya sekta binafsi inayojishughulisha kwenye utalii na kushirikiana
nayo kikamilifu pato la taifa pamoja na ajira za wanaofanya shughuli hizo
zitazidi kudidimia siku hadi siku.
Chimbulo alibainisha kuwa Tanzania imekuwa
ikiwakaribisha wawekezaji na kusajili kampuni za utalii bila kuzifuatilia kwa
ukaribu zaidi, jambo linalochangia kuongezeka kwa kampuni za mifukoni pamoja na
ujangili wa tembo na uhalifu wa rasilimali za taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis
Kagasheki, alikiri kuwa serikali imekuwa na mtazamo usio sahihi kwa kampuni
binafsi za utalii hali iliyochangia kusuasua kwa maendeleo kwenye utalii.
“Tuna sheria nyingi zinazochangia kukwaza sekta ya
utalii, mfano hapa kwetu vibali vya kufanya utalii vinaweza kuchukua hadi miezi
sita wakati wenzetu wa Kenya vinapatikana ndani ya siku zisizozidi mbili, hapa
ni lazima tubadilike ili tujinusuru kwenye anguko hili,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ritta Mlaki (CCM),
alisema serikali imewatelekeza waongoza watalii hapa nchini, hali inayowafanya
wajiongoze kama watoto yatima hatua inayochangia ufanisi na tija kutopatikana
kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya taifa.
“Ndugu zangu wa TATO nyinyi ni watoto lakini
kuanzia sasa tumeamua kushirikiana nanyi, tuleteeni mikakati ya kukuza sekta ya
utalii na sisi tutaishauri na kuisimamia serikali ili tuongeze ajira na fedha
zitakakuza uchumi wetu,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa TATO, Mustapha Akunaay,
alisema wameandaa semina hiyo kwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira pamoja na Kamati ya Bajeti ili waifahamu zaidi sekta ya
utalii na waandae mazingira bora ya kuiboresha kwa lengo la kukuza ajira na
uchumi wa taifa
Chanzo: Tanzania Daima