WATU 30,000 ikiwemo idadi kubwa ya watoto hufa nchini kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotokana na uchafu.
Hayo yalielezwa jana na mratibu wa kampeni ya kitaifa ya Usafi wa
Mazingira, Anyitike Mwakitalima, alipokuwa akitoa taarifa ya kilele cha
kampeni ya unawaji mikono duniani itakayofanyika kitaifa Novemba 19
mwaka huu katika viwanja vya Peoples Club mjini hapa.
Alisema kutokana na watu wengi kutokuwa na uelewa wa umuhimu wa
unawaji mikono kwa sabuni pamoja na matumizi bora ya vyoo, wizara
imeamua kila mwaka kufanya kampeni hiyo ili kuepusha vifo.
Mwakitalima alisema Tanzania inapoteza zaidi ya sh bilioni 13 kwa
mwaka kutokana na kutibu watu wanaougua magonjwa yatokanayo na kuhara
yanayosababishwa na uchafu.
Alieleza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni watekelezaji
wakuu katika suala la usafi wamejipanga kutoa elimu, ili wananchi
wabadilike na waone usafi ni jambo la kuzingatia kwa umakini.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, alisema katika maadhimisho
hayo watafanya Msafara wa Sabuni yenye manufaa kuanzia kwa wanafunzi wa
shule za msingi kwani wao ndio walengwa zaidi.
“Napenda niwaambie ukimfundisha mtoto wakati bado akiwa mdogo akikua
hataweza kukusumbua, hivyo Msafara wa Sabuni unaanzia mashuleni, ili
kuwafunza baadaye wasiweze kuja kufa kwa magonjwa yatokanayo na uchafu,”
alisema Kone.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajia kuwa Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka
huu ni “Usafi ni ustaarabu unaaza na sisi, tumia choo bora, nawa mikono
kwa sabuni, okoa maisha ya watoto”.
Chanzo: Tanzania Daima