Muhongo asusia ndege, akagoma kusafiri na watanzania wenzake daraja la kawaida

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amegoma kusafiri na Watanzania wenzake kwenda nchini Algeria kwa daraja la kaw... thumbnail 1 summary


Mheshimiwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo


WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amegoma kusafiri na Watanzania wenzake kwenda nchini Algeria kwa daraja la kawaida baada ya kukosa daraja la kwanza, hivyo kuahirisha safari yake kwa siku moja, Tanzania Daima limebaini.
Profesa Muhongo ambaye amekuwa akionyesha dharau kwa Watanzania mara kadhaa, aligoma kusafiri katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam Jumapili ya Novemba 24, 2013, saa 10.45 akiwa na wenzake tisa kwenda kwenye safari ya kikazi nchini Algeria alikoenda baadaye.
Moja ya kauli ya dharau iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Muhongo ni pale aliposema wafanyabiashara Watanzania wana uwezo wa kuwekeza kwenye soda na juisi badala ya gesi na pia aliwahi kuwashambulia viongozi wa dini kwa kuwaita waongo.
Uchunguzi wa Tanzania Daima uliofanyika kwa siku kadhaa sasa, umethibitisha kwamba Muhongo alikuwa aondoke na ndege ya shirika la ndege la Emirates namba EK 726 kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kupitia Dubai kwenda Algeria akiwa na tiketi ya daraja la kawaida bila kujua kabla ya kufika uwanjani hapo na kisha kuanza kumfokea kila aliyekuwa anamsemesha.
“Tiketi yake na wenzake kumi ilikuwa ni Economy Class (Daraja la Kawaida), lakini akakataa akitaka asafiri kwa First Class (Daraja la Kwanza). Alibembelezwa na wenzake na wafanyakazi wa Emirates na wale wa Uwanja wa Ndege lakini akagoma huku akifoka na wenzake wakataka kuahirisha safari.
Ikawa tena ni sisi kuwaomba wasafiri ili Bwana Mkubwa (Muhongo) atafutiwe nafasi kwa daraja analotaka.
“Walimbembeleza wakamwambia kwa kutumia ‘millage’ ya safari zake watambadilishia akiwa ndani ya ndege na kumuweka daraja la kwanza lakini alionekana ameshakuwa mkali na hakuwa anamsikiliza yeyote.
“Baadaye tulifanikiwa kuwashawishi wenzake kuendelea na safari na yeye sijui aliondoka na ndege gani tena maana wakubwa wetu wana mambo sana,” anasema ofisa mmoja uwanjani hapo.
Taarifa za awali kuhusu sakata hili, ziliripotiwa siku hiyo katika mtandao wa jamiiforums.com zikieleza kwamba kitendo cha Waziri Muhongo cha kususia safari hiyo, kiliwakera baadhi ya wasafiri wakiwamo raia wa kigeni ambao walishangazwa na hatua hiyo ya kiongozi wa nchi maskini inayotegemea misaada kulazimisha kusafiri kwa daraja la kwanza, daraja ambalo viongozi wa mataifa makubwa hawaruhusiwi kusafiri bila sababu maalumu.
Taarifa hiyo kwenye mtandao wa JamiiForums. Com iliripotiwa hivi: “Kweli viongozi wa nchi hii wanatia aibu, wakati mawaziri wa Uingereza wanakataa First Class, hapa kwetu kimetokea kioja. Waziri wenu wa Nishati na Madini (Muhongo) ambaye anazidi kutulaza na joto na giza leo amewaacha hoi Watanzania pale alipofika mpaka Airport na akiwa anaboard akakuta anawekwa sehemu ya abiria wa daraja la kati, baada ya kuambiwa hayuko First Class akagoma na kutoka nje ya mlango. Wakati hayo yakiendelea kumbe ana wenzake zaidi ya tisa wako economy na wawili Bussiness Class, ghafla nao wakaanza kushuka.
“Hapo ndipo hekima za mmoja wa wahusika wa Airline (Emirates) akawaomba hao waende ili yeye akabadilishe aje kesho yake.”
“Jamani kweli First Class inakushushia aibu hivi Profesa na bado unasema maisha magumu Tanzania!? Inaonekana zile buti za bora ulizivalia ukiwa form V na haya ndio madhara yake, mnapewa vyeo wakati maisha yalishawapiga; mnatafuta muafaka na Yesu mkiwa madarakani,” anaeleza mtu aliyewasilisha mada husika akijulikana kwa jina la Basiasi.
Basiasi alihoji sababu ya abiria wenzake ambao nao walikuwa wakisafiri kikazi kutaka kushuka na kusababisha hasara kwa serikali au wafadhili waliokata tiketi hizo.
Kwa utaratibu wa kawaida abiria anayeahirisha safari baada ya kuwa ameshaingia ndani ya eneo la kusafiria (boarding) anaweza kupoteza kabisa tiketi au kulipishwa fedha nyingi zinazoweza kuwa sawa na kununua tiketi mpya.
“Hebu kuweni wastaarabu, sasa wale watu tisa walitaka kuwashusha kwa nini na kama wamekwenda, mlishindwa kuwaambia wabaki mpaka mkaanza kuleta aibu uwanjani? Inaonekena ndege mmeanza kupanda uzeeni; najiuliza kivipi unaletewa tiketi hata kama na ‘travel agency’ halafu unashindwa kuuliza au kukagua mpaka unaenda uwanjani na unapewa ‘boarding pass’ bado unashindwa kukagua ipi ‘bussiness class’ na ipi ‘first class’!” anahoji Basiasi.
Abiria mmoja aliyenukuliwa na Jamiiforums alisema kwa waziri wa nchi kama Uingereza anatakiwa kutoa maelezo ya sababu za kusafiri na daraja la kwanza (first class) ikiwa atalazimika kufanya hivyo, vingine viongozi husafiri kwa madaraja ya kawaida.
Wakati Waziri Muhongo akisusia ndege kwa kukosa nafasi ya kusafiri na daraja la kwanza, baadhi ya mawaziri wanaofanya ziara mikoani na kusafiri kwa ndege, hulazimika kuyaagiza mashangingi yao kutoka Dar es Salaam hadi katika mikoa wanayokwenda kufanya ziara hizo hata kama yatatumika kwa siku moja.
Chanzo: Tanzania Daima