Rubani wa ndege ya Auric Air Abel |
Novemba
15 mwaka 2013 Shirika la ndege la Auric Air lilianzisha
safari mpya za ndege za kila siku kati ya Dar es Salaam na Morogoro ikiwa ni
mipango yake ya kuwafikia wananchi wengi katika mikoa mbalimbali Tanzania.
Actually, toka safari
hizo zianze sikuwahi kupata nafasi ya kusafiri nao, lakini hivi
majuzi tu nikitokea Dodoma kwa basi niliamua kushuka Morogoro kutekeleza
majukumu yangu kadhaa. Kesho yake nilikuwa na kibarua kingine huko Dar es
Salaam tena asubuhi na mapema hivyo niliona njia pekee ya kuwahi miadi yangu
kutoka Morogoro ni kutumia usafiri wa ndege.
Kesho yake asubuhi
nikaelekea uwanja wa ndege wa Morogoro ambao kwa kweli watu wengi hawafahamu
ulipo. Hilo lilidhihirishwa na dereva tax aliyenipeleka uwanja huo, maana
alikuwa hajui geti la kuingilia uwanjani hapo jambo lililofanya tuzunguke huku
na kule kutafuta geti la kuingilia.
Hata tulipowauliza
watu wanaoishi maeneo ya modeko karibu na uwanja huo nao hawakujua geti lilipo
(hapa inabidi kufanyike matangazo ya kutosha na kuweka bando kubwa kwenye
barabara ya kuingia uwanjani hapo). Lakini hatimaye tulifanikiwa kufika kwa
wakati na kuketi kusubiri muda wa kuondoka ndege.
Nikiwa uwanjani hapo
nilikutana na bwana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Benard Myinga ambaye ni
Afisa Ugavi kutoka Tanzania Tree Seeds Agents, wasambazaji wa mbegu za miti, ambaye
alieleza mtazamo wake kuhusu usafiri huo mpya wa ndege katika mji kasoro
bahari.
“Hakika ni jambo jema
kupata usafiri wa ndege hapa Morogoro, unajua kuna watu wengi wanamahitaji ya
kufanya safari za haraka za kibiashara, matibabu na mapumziko lakini kwa muda
mrefu kumekuwa hakuna huduma hiyo” anasema na kuongeza:
“Mfano sasa nakwenda
Dar kwa matibabu ya mkono wangu ambao ulivunjika kwenye ajali ya gari
nikielekea Iringa, nimekuwa nikipata tabu sana kupanda mabasi mpaka dar kwa
matibabu, kwanza inachukua muda mrefu, pili mkono unarushwarushwa hivyo
kuniongezea maumivu lakini inaniongezea gharama maana nikienda kwa basi siwezi
kurudi siku hiyohiyo na lazimika kulipia hoteli”
Kwa maelezo hayo
mafupi nilipata picha ni kwa namna gani usafiri wa ndege utakuwa msaada mkubwa
kwa wanamorogoro, hasa katika kukuza uchumi, maendeleo na kuwezesha mipango ya
mji huo kuwa jiji.
Safari yangu ilikuwa
nzuri maana nilitumia saa moja kufika Dar es Salaam na kuwahi kufanya mambo
yangu, hakika auric air ni mkombozi wa usafiri wa ndege Morogoro na habari
njema nyingine ni kwamba very soon wataanzisha safari kati ya Dar-Dodoma (bado
chini ya kapeti)
Morogoro kutokea angani
Ni
hayo kwa leo, nitakuja na simulizi nzima ya kila hatua ya yale
niliyojifunza na yanayozungumzwa kuhusu Auric Air, endelea kuwa nami