Mkataba mpya wa mazingira na INDCs vitafunga au kufungua njia za uchumi Tanzania?

RoadToParis2015 with tabianchiblog&CFIMedias21 SIASA! SIASA! SIASA! Imekuwa ni wimbo wenye kibwagizo kinachokoleza toka kuanza kw... thumbnail 1 summary
RoadToParis2015 with tabianchiblog&CFIMedias21

SIASA! SIASA! SIASA! Imekuwa ni wimbo wenye kibwagizo kinachokoleza toka kuanza kwa mwaka huu wa 2015, hii ni kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hili ni jambo jema kwa nchi yenye kufuata mfumo wa demokrasia na unaozingatia haki za watu kuchagua viongozi wanaowataka au kuchaguliwa kuwa viongozi.
Harakati hizi za uchaguzi zimegeuza akili, nguvu, maarifa na hata mawazo ya watu wengi kiasi tumesahau kuwekea manani mambo mengine ya msingi na yanayogusa pia maisha yetu ya kila siku.
Mbali na uchaguzi mkuu, mwaka huu pia kutakuwa na jambo kubwa na la kimataifa ambao ni Mkutano wa ishirini na moja (COP21) wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ambao utafanyika jijini Paris, Ufaransa mwezi disemba mwaka huu.

Heka heka unazoziona kwenye kampeni za wagombea kujinadi na kutoa ahadi watakazowafanyia wananchi endapo watapewa dhamana ya kuwaongoza ziko pia kwenye mchakato wa kuelekea kwenye mkutano huo wa Paris mwaka huu.

Utofauti wa mambo haya mawili ni kwamba ahadi za uchaguzi zinaitwa KAMPENI lakini za COP21 zenyewe zinaitwa INDCs. Umewahi kusikia kuhusu INDCs?  Ni mchango wa kila nchi katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined Contributions – INDCs)

Kwenye Mkutano wa ishirini wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi huko Lima, Peru ambapo Tanzania pia ilishiriki, yalifanyika makubaliano ya kila nchi kuandaa na kuwasilisha maeneo maalumu yatakayokuwa ni mchango wa nchi husika katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (INDCs).

Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na wadau, Tanzania kwa sasa inafanya mchanganuo wa maeneo muhimu yatakayokuwa ni mchango wa Tanzania katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo kazi ya kuandaa INDCs inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu, na kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya Mkataba.

Ni jambo la kupongeza kwa Tanzania kuanza mchakato wa INDCs lakini ni muhimu pia kujua maana na umuhimu wa INDCs na kutafakari kwa kina kama zina faida au madhara kabla ya kuwasilisha panapohusika.

Mchakato huo kwa kiasi kidogo sana umewashirikisha wananchi wa Tanzania hasa wale walioko kwenye sekta zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kama vile kilimo, afya na uvuvi.

Ikumbukwe kuwa Tanzania ndo kwanza imevumbua gesi na mafuta, je huu ni wakati muafaka wa kuingia kwenye mkataba huu wa INDCs? Mkataba ambao unaweza kulazimisha nchi changa kiuchumi kama yetu kupunguza shughuli za kukuza uchumi zenye viashiria vya kuharibu mazingira.

Je, kuna ulazima gani wa nchi kuingia kwenye mkataba huu? Serikali yetu imejipangaje kusimamia na kutekeleza ahadi zitakazokuwa kwenye hiyo INDCs? Yaliyomo kwenye mkataba huo yanafaida gani kwa jamii? Wadau wameshirikishwa kwa kiasi gani wakati wa mchakato?

Majibu ya maswali haya yatatoa mwanga kwa mtanzania wa kawaida, kujua nchi yake inakwenda kuingia kwenye mkataba kwa manufaa au madhara yapi ili aweze pia kushiriki katika utekelezaji wake.

Kabla ya Serikali yetu haijakwenda kushiriki kikamilifu katika majadiliano ili kupata Mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi ambao unatarajiwa kupitishwa mjini Paris mwezi Desemba, 2015, ni lazima itoe majibu yanayojitosheleza, ijitathmin na kujiridhisha kuwa inauweza wa kutunza ahadi na kuyasimamia iliyoyapanga.

COP21 ni muhimu sana kwa sababu utashirikisha nchi 196 ambao ni washiriki wa umoja wa mataifa kote duniani kuhakikisha kuwa shughuli za maendeleo hazisababishi joto la dunia kuongezeka kwa zaidi ya nyuzijoto mbili (2oC) juu ya kiwango cha sasa, ili kuepuka madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa binadamu na viumbe wengine.

Aidha, Mkataba utatoa fursa kwa nchi ambazo tayari zinaathiriwa na mabadiliko ya  tabianchi kupewe fedha, teknolojia na kujengewa uwezo wa kuhimili mabidiliko ya tabianchi katika nyanja zote.