Mbunge ataka sheria ndogo za vijiji kutunza mazingira Ziwa Rukwa

Na Walter Mguluchuyma Mpanda. MBUNGE wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha amewashauri viongozi wa vijiji vya ukanda wa bonde la ziwa Rukwa... thumbnail 1 summary
Na Walter Mguluchuyma

Mpanda.

MBUNGE wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha amewashauri viongozi wa vijiji vya ukanda wa bonde la ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa kutunga sheria ndogo ndogo za kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanywa kwenye  ziwa Rukwa ili kunusuru lisikauke katika kipindi kifupi kijacho.

Mbunge Malocha alisema hayo jana wakati wa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Uzia kata ya Muze wilayani Sumbawanga wakati wa ziara yake ya kuhamasisha shughuli za maendeleo anayoifanya jimboni kwake kufuatia kuulizwa swali na mwananchi mmoja aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani kudhibiti hali hiyo.

Mwananchi aliyefahamika kwa jina la Gerald Komba alihoji kwanini Serikali isibebe lawama iwapo ziwa hilo litakauka kwa kuwa hakuna hatua za makusudi zinazooneka kufanyika kupambana na uharibifu mazingira ambao unatishia ziwa hilo kukauka.

Akijibu swali hilo, Malocha alisema kuwa wataalamu wa mazingira wamedai kuwa Ziwa hilo halina miaka 20 mbele linaweza kukauka iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanyika kwenye ziwa hilo hivyo Serikali za vijiji kwa kushirikiana na Halmashauri zinapaswa kutunga sheria ndogo ndogo kudhibiti uharibifu katika ziwa hilo.

Malocha alisema kuwa kutokana na uharibifu mazingira katika ziwa hilo ambao umechangia udongo kuingia ndani kwa zaidi ya kilometa saba kuelekea kwenye kina cha ziwa pia ipo haja shughuli za uvuvi zisimamishwe kwa muda kwa kuwa matumizi ya kibinadamu kama uvuvi nayo yamesababisha kutokea hali hiyo.

"mie siwezi kusema simamisheni uvuvi kwa muda.....lakini kama uvuvi unasababisha uharibifu wa mazingira na vijiji na kata ziwasilishe mapendekezo yao katika halmashauri husika ili ione umuhimu wa kusimamisha kwa muda shughuli za uvivu" alisema Malocha.

Aidha, aliwashauri viongozi wa vijiji kutenga maeneo ya malisho sambamba na kutunga sheria itakayowabana wafugaji kutokuwa na idadi kubwa ya mifugo kwani wingi wa mifugo umekuwa ukisababisha kukosa maeneo ya malisho hivyo kulisha kwenye mashamba ya wakulima hali inayosababisha mapigano baina ya pande hizo mbili.

Kwa kipindi kirefu bonde la ziwa Rukwa limekuwa na migogoro baina ya wafugaji na wakulima inayosababishwa na wingi mifugo ambayo inayokosa maeneo ya malisho hivyo kulishwa ndani mashamba ya wakulima.