SERIKALI mkoani Mbeya imetishia kukatisha
mikataba ya madaktari watakaoendeleza mgomo mpaka siku ya kesho(Juni 27) ikiwa
ni siku tano mfululizo hawajaingia kazini.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Mbeya Dk.Norman Fegi
ameyasema hayo leo (Juni 26) katika kikao chake na waandishi wa habari ikiwa ni
siku ya nne mfululizo tangu baadhi ya madaktari katika hospitali ya Rufaa
kuanza mgomo.
Dk.Fegi amesema tangu kuanza kwa mgomo huo
serikali ya mkoa kupitia mkuu wa mkoa ambaye kisheria ndiye mwenyekiti wa bodi
ya hospitali inayoingia mkataba na madaktari wa mafunzo imeshawaandikia barua
za kuwaita ili wafanye mazungumzo lakini jana(Juni 25) hawakufika.
Amesema baada ya kutofika huko mkoa
ukawaandikia tena barua kwa kila mmoja wao kujibui ni kwa nini asiwajibishwe na
kusisitiza kuwa iwapo mpaka siku ya tano hawatafika kazini mkoa utavunja
mkataba na kuwarudisha kwa muajiri yaani wizara husika.
Amesema kwa sasa wamelazimika kuchukua baadhi
ya madaktari kutoka vituo vya afya vilivyopo jijini Mbeya na ndiyo wanaendelea
kutoa huduma hususani katika kitengo cha upasuaji cha hospitali ya Rufaa
ambacho ndicho kimeathiriwa zaidi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa hospitali ya
mkoa Dk.Eliuter Samky alisema madaktari waliogoma ni 45 waliopo katika mafunzo
na 19 waliosajiriwa lakini wameajiriwa hivi karibuni lakini madaktari bingwa 19
wanaendelea na kazi kama kawaida.
Samky amesema wateja wote waliofika
hospitalini hapo tangu kuanza kwa mgomo wameathirika kwa namna moja ama
nyingine ikiwa ni kwakupata huduma isiyo katika kiwango ama muda wa kawaida au
kisaikolojia.
Amesema tangu kuanza kwa mgomo huo haijatokea
kifo lakini wagonjwa 250 wamefikishwa na kulazwa wakati wagonjwa wan je
jumamosi walifika 53,jumapili 42 na jumatatu 283.
Amesema siku ya jumapili pia ilitokea ajali ya
gari na majeruhi 16 wakafikishwa hospitalini hapo na wote walipata huduma japo
si kwa kiwango kilichozoeleka siku zote.
Naye mganga mkuu wa mkoa dokta Seif Mhina
alisema mgomo wa madaktari katika hospitali ya rufaa imeongeza msongamano wa
wagonjwa katika hospitali ya mkoa hususani akina mama wajawazito waliokwenda
kujifungua katika hospitali hiyo kitengo cha wazazi Meta na kukosa huduma ndipo
wakaamua kukimbilia hapo.
Mhina amesema wajawazito wanaojifungua katika
hospitali ya mkoa wameongezeka kutoka wawili hadi watano kwa siku na kufikia
zaidi ya kumi huku wanaopata huduma ya upasuaji wakiongezeka kutoka mmoja kwa
siku hadi kati ya watano na kumi.
Chanzo: Jodanyp blog