WANACHAMA
wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wametakiwa kutochagua viongozi kwa nafasi zao za
kifedha wanazozitumia kurubuni wananchi kwa kutoa misaada mingi na kujinadi makanisani kila kukicha.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye
ametoa kauli hiyo leo (Juni 26) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
jijini Mbeya kauli inayoonekana kumhusu moja kwa moja aliyewahi kuwa Waziri
mkuu Edward Lowasa ambaye hivi sasa anaonekana kukimbilia makanisani kwa
kuchangia harambee mbalimbali.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo hususani ya
kisiasa wamekuwa wakiitaja njia anayoitumia Lowasa kuwa njia ya kujisafisha na
kujitengenezea nafasi nzuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Lakini Nape amesema wanaccm wanapaswa wautumie
uchaguzi wa chama chao mwaka huu kuhakikisha viongozi wanaomwaga pesa nyingi
kwa kutoa misaada wakidhani ni njia nzuri ya kuwashika wapiga kura wanatupwa
nje ili kukisafisha chama chao.
Amesema kinachopaswa kufanywa na wanachama ni
kuhakikisha wanachagua viongozi walio na uzalendo na chama chao na pia walio na
uwezo wa uongozi ili kukijenga chama hicho badala ya kuwapa uongozi watu
wanaonyooshewa vidole kila siku na wananchi.
Amewataka vijana hususani walio na elimu
kujitosa kupigania uongozi wa chama hicho akisema hatua hiyo itakiwezesha
kupata damu change na zilizo na nguvu ya kukiendeleza badala ya kukidumaza.
Nnauye amekanusha pia kauli za baadhi ya watu
wanaokejeli dhana ya Kujivua Gamba wakisema haijafanikiwa kauli aliyosema si
kweli kwani dhana hiyo ilibeba mambo mengi ndani yake.
Amesema dhana hiyo ililenga kubadilisura ya
chama kwa kuongeza damu change hali inayofanyika hivi sasa ambapo chama
kimeanzisha mchakato wa kuwa nam mkoa maalumu kwaajili ya wanafunzi wa vyuo vya
elimu ya juu.
Amesema pia kuwawajibisha baadhi ya viongozi
wasio na sifa tayari mikakati mbalimbali imefanywa na wapo baadhi ya watu
walioachia ngazi mbalimbali pamoja na kuivunja kamati kuu iliyokuwa chini ya
Yusuf Makamba.
“Kuna watu wamejivua uanachama mpaka ubunge
tumeona leo hii mtu anasema dhana ya Kujivua Gamba haijafanikiwa mi nadhani ni
uongo.Lakini pia baada ya chama kutoa muda kwa wahusika wajiwajibishe na
hawakufanya hivyo sasa tuna vikao mbalimbali vinavyoendelea kpitia kamati za
maamuzi na maadili.Huko nako tutatoka na maamuzi mengine” amesema.
Amesema pia katika uchaguzi mkuu wa chama
hicho mwaka huu majina ya wagombea wanaokabiliwa na kashfa mbalimbali
hayatarejeshwa hivyo ni vema wanachama hao wasijaze fomu kabisa.
Chanzo: Jodanyp blog