Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kama linavyoonekana pichani.
Ofisa Tabibu wa Kituo cha Afya Songwa, Bundala Nandule.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Kishapu
Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya
Kishapu mkoani Shinyanga kimekatiwa umeme kwa takribani miezi saba sasa
kikidaiwa bili ya umeme na TANESCO ya jumla ya sh. 38,000 hali inayowabebesha
mzigo wa gharama wananchi wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Wagonjwa wanaotibiwa usiku katika kituo hicho hasa
wanawake wajawazito wanalazimika kugharamia mafuta ya taa kwenye chemli za
kituo au kuchangia sh. 1200 kabla ya huduma yoyoto ili kupatikana mwanga
unaowawezesha wahudumu kufanya kazi zao usiku.
Akizungumza na Thehabari.com kijijini Songwa,
Jamila Nyalulu mkazi wa eneo hilo alisema wananchi wasio na uwezo wa kuchangia
mafuta ya taa hasa kwa huduma za uzazi wamekuwa wakipata tabu, jambo ambalo
limekuwa likihatarisha maisha yao kiafya.
Ofisa Tabibu wa Kituo hicho, Bundala Nandule
amekiri hali hiyo inakwamisha ufanisi wa utoaji huduma za afya hasa kwa
wagonjwa wa usiku au wanaopumzishwa na kuongeza kuwa tarari wameripoti suala
hilo katika uongozi wa Halmashauri ya Kishapu lakini bado linafanyiwa kazi.
“Tatizo la umeme linatusumbua kwa kweli hasa
mgonjwa anapokuja kupata huduma usiku. Wagonjwa wa kawaida hulazimika kuja na
tochi, lakini kwa wajawazito wanatakiwa kuja na fanta moja (chupa ya soda) ya
mafuta ya taa au aje na sh. 1200 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kabla ya
huduma,” alisema Nandule.
Hata hivyo akizungumzia tatizo hilo, Kaimu
Mkurugenzi wa Wilaya ya Kishapu, Lucas Said alisema wanamshangaa Mkuu wa Kituo
hicho cha afya kushindwa kufuatilia malipo ya bili katika ofisi za halmashauri
kwani cheki ya malipo ya bili hiyo iliandikwa tangu mwaka jana (2011).
“Kituo hicho kilikuwa kinadaiwa sh. 38,000 na cheki
iliandikwa tangu mwaka jana lakini wahusika hawajatokea ili wakabidhiwe cheki
hiyo…huu ni uzembe,” alisema kiongozi huyo wa Halmashauri ya Kishapu.
Kituo cha afya cha Songwa kinatoa huduma kwa zaidi
ya vijiji vitatu vya Wilaya ya Kishapu, ambavyo ni pamoja na Kijiji cha Songwa,
Bushola, Seseko na baadhi ya zahanati zilizopo jirani na kituo hicho.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com
(www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP).