Kesi 200 za ardhi zafunguliwa Kinondoni

Na Simon Nyalobi, Dar es Salaam   ZAIDI ya wakazi 200 wa Wilaya ya Kinondoni wamefungua kesi mbalimbali za kuvamiwa maeneo yao kinyume c... thumbnail 1 summary
Na Simon Nyalobi, Dar es Salaam
 
ZAIDI ya wakazi 200 wa Wilaya ya Kinondoni wamefungua kesi mbalimbali za kuvamiwa maeneo yao kinyume cha sheria katika Baraza la Nyumba na Ardhi la Wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alipozungumza na MTANZANIA ofisini kwake, baada ya kutoka katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama cha wilaya hiyo, kilichozungumzia kwa kina migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.

“Wakazi 200 wamefungua kesi katika Baraza la Nyumba na Ardhi la Wilaya wakilalamikia kuvamiwa maeneo yao na tunataka wananchi wengine wajitokeze kufungua kesi hizo, ili kuondoa usumbufu wa migogoro hiyo, badala ya kukaa na kulalamika pekee,” alisema Rugimbana.

“Tunataka wananchi wafanye hivyo, wafungue katika Baraza la Wilaya na siyo Kata, wilaya sasa imeamua kulishughulikia suala hilo baada ya hukumu kutolewa na baraza na sisi tutatekeleza maamuzi hayo, kama unavyojua sisi ndiyo wenye mamlaka ya utekelezaji, wao baraza wanatoa maamuzi tu,” alisema Rugimbana.

Hata hivyo amewataka wavamizi wa maeneo yasiyokuwa yao kisheria kuhama haraka kabla uongozi wa wilaya hiyo haujaanza mchakato wa kubomoa nyumba zao.

Alisema baada ya Baraza la Nyumba na Ardhi la Wilaya kutoa maamuzi ya nani mmiliki halali wa eneo husika, uongozi wa wilaya utachukua hatua za haraka katika kuwaondoa waliovamia maeneo hayo.

Rugimbana, ambaye pia ni Mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema wameamua kwa dhati kupambana na kero za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero ya muda mrefu.

Chanzo: Mtanzania