TANAPA yajipanga kukabili ujangili

na Ghisa Abby, Morogoro   SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limesema kuwa wanyamapori na maliasili za taifa katika hifadhi mbalimb... thumbnail 1 summary

na Ghisa Abby, Morogoro
 
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limesema kuwa wanyamapori na maliasili za taifa katika hifadhi mbalimbali nchini zimeendelea kuwa kwenye hatari kubwa kutokana na mbinu za kiinterijensia na silaha za kivita zinazotumiwa na majangili.

Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya askari wa wanyamapori katika Chuo cha maofisa wa Jeshi la Polisi Kidatu mkoani Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi, alisema kuwa rasilimali za taifa  wakiwamo wanyamapori wamekuwa katika hatari kubwa kutokana na ujuzi mkubwa wa majangili kwa sasa.

Aliwatataka askari wa TANAPA kuongeza ujuzi na mbinu za kiinterijensia katika kupata taarifa sahihi za majangili kwani wengi wao wameachana na matumizi ya silaha za kijadi na badala yake wanatumia silaha za kivita.

Kijazi alisema kuwa pamoja na TANAPA kukabiliwa na changamoto mbalimbali ndiyo maana imeona kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa mafunzo kwa askari wake.

“Aina za mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya polisi yamekuwa yakikidhi matakwa yetu ya kukabiliana na ujangili uliopo sasa,” alisema Kijazi.

Naye mgeni rasmi katika mafunzo hayo, Mkuu wa mafunzo wa Jeshi la Polisi makao makuu, Elice Mapunda, alisema kuwa usalama wa hifadhi za taifa  umekuwa ukiwategemea wao, kwamba ni vema kutumia mafunzo hayo kwa faida ya taifa.

Mapunda aliwataka askari hao kuachana na dhana ya kizamani kuwa watu wanaofanya uhalifu katika maeneo ya nchi na hata kwenye hifadhi ni wale wasiokuwa na elimu ya kutosha.

Naye mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Polisi Kidatu, Nasser Mwakambunja, alisema kuwa wahitimu hao, wamefundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukakamavu na kuzingatia haki za binadamu katika utendaji wao.

Jumla ya wahitimu 66  wamehitimu mafunzo katika  upelelezi wa awali wa kughushi hati na kuiba, wizi wa mtandao na namna ya kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali.

Chanzo: Tanzania Daima