na Walter Mguluchuma, Mpanda
SHULE za msingi za Mnyamasi na Moto zilizopo wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, zinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo walimu kuishi katika vyumba vya madarasa huku wanafunzi wakisomea chini ya miti.
Haya yalibainika wakati wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Ngemela Lubinga, katika kata za Nsimbo na Mamba kwaajili ya kujitambulisha, kukagua miradi ya maedeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majimoto, Delamu Binde alimfahamisha mkuu huyo kuwa kutokana na uhaba wa vyumba za walimu katika Shule ya Msingi Mnyamasi, walimu wanne wamelazimika kuishi katika vyumba vya madarasa shuleni hapo.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Msingi Namasi, mkuu huyo wa shule, alisema kuwa shule hiyo yenye walimu sita wa kiume, wanne kati yao wamelazimika kuishi katika vyumba vya madarasa.
Binde aliongeza kuwa wanafunzi wa shule hizo za Majimoto na Mnyamasi, wanasomea chini ya miti kufuatia uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa na madawati unaozikabili.
“Shule ya Msingi Majimoto ina wanafunzi 1,661 na kati yao 420 tu ndio wanakalia madawati huku wengine 1,241 wakilazimika kukaa chini,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Marius Nazi, alisema kuwa tayari ofisi hiyo imeshatengeneza madawati zaidi ya 7,000 ambayo yatagawiwa katika mbalimbali hivi karibuni ili kukabiliana na kadhia hiyo ya upungufu.
Ili kuondokana na adha ya walimu kuishi katika vyumba vya madarasa, alisema tayari ofisi yake imetengewa zaidi ya sh milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu shuleni hapo.
Chanzo: Tanzania Daima